Kurasa Muhimu

Tuesday, October 30, 2012

RIPOTI YA KONGAMANO LA KISWAHILI LILILOFANYIKA BURUNDI

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

TAASISI YA TAALUMA ZA KISWAHILI





CHAMA CHA WANAFUNZI WA KISWAHILI VYUO VIKUU AFRIKA MASHARIKI TAWI LA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM (CHAWAKAMA-UDSM)




RIPOTI YA KONGAMANO LA 8 LA KISWAHILI LILILOFANYIKA BURUNDI.


Yaliyomo       


Shukurani

Tunapenda kutoa shukurani zetu za dhati kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa moyo wao wa kusaidia waliouonesha kwetu. Hawakuwa na kitu lakini walitusaidia kiasi kidogo  cha fedha ambacho kwa kweli kilitusaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha safari yetu, ikizingatiwa kwamba ndio wafadhili  pekee waliojitokeza kutusaidia, kwa kweli tunawashukuru sana.
Pia tunawashukuru TATAKI kwa kuwa karibu nasi, wamekuwa wakitutia moyo katika shughuli zetu, pia wamekuwa wakifuatilia kwa ukaribu sana shughuli zetu, vilevile TATAKI ndio wamekuwa wafadhili wetu wakuu wakati tunapokuwa na kongamano au shughuli nyingine za kiswahili. Tunathamini jitihada zao katika kuimarisha CHAWAKAMA hapa chuoni.
Mwisho tunapenda kuwashukuru wale wote waliotusaidia kwa namna moja ama nyingine katika  kufanikisha kuhudhuria kongamano, bila kuwasahau kampuni ya Vodacom ambao kwa kweli walionesha nia ya kutusaidia ingawaje hawakuweza kwa wakati huo. Tunasema asante kwa kuonesha kuwa mnatujali.

Utangulizi
Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili  vyuo vikuu Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kilianzishwa mwaka 2004; toka kilipoanzishwa kimekuwa na utaratibu wa kuandaa makongamano kila mwaka. Utaratibu huu unazingatia ushirikiswaji wa nchi husika, kwa maana kwamba kila nchi inapewa jukumu la kuandaa kongamano na ni haki ya msingi kwa nchi wanachama kwa mujibu wa katiba ya chama.
Pamoja na utaratibu wa chama kuandaa makongamano pia uanzishwaji wake umeambatana na malengo kadhaa ambayo ndiyo dira inayoiongoza chama kwa mujibu wa katiba, malengo hayo ni haya yafuatayo:
i.Kuwapa wanachama nafasi ya kujadili, kuimarisha, kuendeleza na kukuza vipawa vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili.
ii.Kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa lugha ya kiswahili.
iii.Kueneza lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi.
iv.Kushirikiana na vyama vingine katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha      lugha ya kiswahili ndani na nje ya nchi wanachama.
v.Kuwaunganisha wanafunzi wa kiswahili Afrika Mashariki na kati katika kukikuza kiswahili.
vi.Kushirikiana na asasi mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa kiswahili ndani na nje ya nchi kama vile BAKITA, TATAKI, TAKILUKI, UWAVITA, CHAKAMA, BAKIZA n.k.
vii.Kuchapisha kijarida cha chama na machapisho mengine ili kusaidia kueneza taaluma ya kiswahili.
viii.Kuweka kumbukumbu ya wataalamu wa kiswahili kwa nia ya kuwatumia katika kufanikisha malengo ya chama na wadau wa kiswahili.
ix.Kuratibu makongamano na mijadala mbalimbali inayohusiana na taaluma ya kiswahili.
Kwa kuzingatia utaratibu wa chama wa kuratibu na kuandaa makongamano, kongamano la mwaka huu limefanyika nchini Burundi. Kwa kutambua umuhimu wa kongamano hili na katika kutimiza jukumu letu, sisi CHAWAKAMA tawi la Chuo kikuu cha Dar es salaam (CHAWAKAMA-UDSM)  tulipanga kwa dhamira ya dhati kuhudhuria licha ya changamoto ya ukosefu wa fedha tuliokuwa tukiukabili. Kuhakikisha tunaitatua changamoto hii tuliamua kuzunguka kwa wafadhili mbalimbali wakiwamo BAKITA ambao kwa kweli ndio waliochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha safari yetu.
Wanachama kutoka Chuo kikuu Cha Dar es salaam tuliohudhuria tulikuwa jumla ya watu kumi na mmoja, viongozi wakiwa watano na na wanachama wakawaida 6 , idadi hii ni ndogo kulinganisha na idada ya wanachama tulionao katika tawi letu. Kwa hiyo ripoti hii inalenga kuelezea yale yaliyotokea katika kongamano lililofanyika Burundi Agosti 30 – Septemba 1 mwaka 2012 na kuelezea hali ya Kiswahili nchini Burundi na mwisho ni hitimisho pamoja na mapendekezo.

Kongamano lenyewe

Kongamano la 8 la kimataifa la lugha ya kiswahili mwaka 2012 lililoandaliwa na CHAWAKAMA wakishirikiana na chama cha kiswahili nchini Burundi (SAPROSS) ambao ndio waliokuwa wenyeji wa mkutano lilifanyika katika shule ya Don Bosco mjini Ngozi kaskazini mwa Burundi. Washiriki wa kongamano walianza kuwasili tarehe 29 Agosti kutokea katika vyuo mbalimbali vya Afrika mashariki kikiwamo Chuo kikuu cha Dar es salaam kikiwakiliswa na washiriki kumi na mmoja. Jioni ya siku hiyo tulipokelewa vizuri na wenyeji wa kongamano na tukatumia muda huo kwa ajili ya kujiandaa na ufunguzi rasmi wa kongamano kwa siku iliyokuwa inafuata, kwa hiyo siku ya kuwasili hatukufanya kitu chochote kinachohusiana na kongamano.
Siku ya tarehe 30 Agosti ndio ilikuwa siku rasmi kwa ajili ya ufunguzi wa kongamano. Kabla ya ufunguzi rasmi tuliingia ukumbini kwa maandamano huku nyimbo nzuri za kukitukuza chama na kiswahili kwa ujumla ziliimbwa kwa umakini kabisa na watu wote walionesha hamasa ya hali ya juu huku wakiimba nyimbo hizo kwa furaha na uchangamfu mkubwa. Baada ya kuingia ukumbini tuliketi wote kwa utulivu na kuendelea kusikiliza kile kitakachofuata.
Ilipofika saa tano asubuhi kongamano likawa limefunguliwa rasmi, na mgeni rasmi wa kongamano alikuwa ni Mshauri wa elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ufundi wa nchi ya Burundi. Baada ya ufunguzi huo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa.

Washiriki wa kongamano

Kongamano hili lilikuwa na washiriki (wahadhiri pamoja na wanafunzi) kutoka katika vyuo mbalimbali vya Afrika Mashariki yaani vyuo kutoka Burundi, Rwanda, Uganda, Tanzania na Kenya. Vyuo vilivyoshiriki katika kongamano la 8 kutoka nchi hizi ni:
  1. Chuo kikuu cha Dar es salaam (Tanzania)
  2. Chuo kikuu cha Mtakatifu Agostino (Tanzania)
  3.  Chuo kikuu cha Makumira (Tanzania)
  4. Chuo kikuu kishiriki cha Ruaha [RUCO] (Tanzania) 
  5.  Chuo kikuu cha Kiislam Morogoro[MUM] (Tanzania) 
  6.  Chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania (Tanzania) 
  7.  Chuo kikuu kishiriki cha Mkwawa (Tanzania 
  8.  Chuo kikuu cha Moi (Kenya) 
  9.  Chuo kikuu cha Elimu cha Kigali (Rwanda)  
  10.  Chuo kikuu cha Maseno (Kenya) 
  11. Chuo kikuu cha Burundi (Burundi) 
  12.  Chuo kikuu cha Arusha (Tanzania) 
  13. Chuo kikuu cha Bishop Stuart (Uganda)
Jumla ya makala 15 ziliwasilishwa na washiriki kutoka vyuo mbalimbali, mada hizo hatutazijumuisha katika taarifa hii na badala yake baadhi ya makala tutazichapisha katika jarida letu liitwalo Zinduko. Katika taarifa hii tutapata fursa ya kuona mada tu za makala zilizowasiliswa katika kongamano hilo, mada hizo ni hizi zifuatazo:
    • Maendeleo ya Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).  Mwasilishaji ni Aritamba Malagira, Chuo kikuu cha Dar es salaam.
    • Nafasi ya Kiswahili katika uchumi, siasa, utamaduni na michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki. Mwasilishaji ni Majula Kutoka SAUT Mwanza.
    • Ufundishaji, ukuaji, mafanikio na changamoto, zinazoikabili lugha ya kiswahili nchini Tanzania.  Sineda Kadaso kutoka SAUT Tabora.
    • Nafasi ya Kiswahili katika utandawazi. Mwasilishaji ni Owino Ochola na Anne Mwari kutoka Moi –     Kenya.
    • Nafasi ya Kiswahili katika uchumi, siasa na utamaduni. Mwasilishaji kutoka Kenya.
    • Shairi – Lugha yetu.Mwasilishaji ni Ekiru Simon kutoka Moi.
    •  Nafasi ya Kiswahili nchini Rwanda. Mwasilishaji ni Niyirora Emmanuel kutoka Chuo kikuu cha Elimu cha Kigali.
    • Shairi – Kiswahili ni hazina. Mwasilishaji ni Mercy Agwanda kutoka Chuo kikuu cha Maseno.
    • Shairi – Karibu Burundi. Mwasilishaji ni Maurice Berahino kutoka Chuo kikuu cha Burundi.
    • Nadharia ya ujumi mweusi katika ushairi wa Kiswahili. Mwasilishaji ni Tumaini J. Sanga, Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Mtakatifu Yohana – Tanzania.
    • Lugha ya Kiswahili ilianza katika ombwe na chimbuko lake ni utata. Unasemaje? Mwasilishaji ni Edina Bilishanga, Chuo kikuu cha Dar es salaam.
    • Kiswahili kinafaa kuwa lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu nchini Tanzania. Mwasilishaji ni Theresia B. Mbogo, Chuo kikuu cha Dar es salaam.
    • Ufundishaji, ukuaji, mafanikio na changamoto zinazoikabili lugha ya Kiswahili nchini Burundi. Mwasilishaji ni Nshimimana Dorothee, Mhadhiri, Chuo kikuu cha Burundi.
    • Bembelezi. Mwasilishaji ni Fidelis K. Kyarwenda, Chuo kikuu cha Arusha.
    •  Pambo la Kiswahili. Mwasilishaji ni Fredrick Kamayugi, Tanzania.
Siku ya tarehe 1 Septemba asubuhi wanachawakama wote tulikusanyika kwa ajili ya shughuli za kijamii. Kwa mujibu wa sheria za nchi ya Burundi kila siku ya jumamosi ni siku maalumu kwa ajili ya shughuli za kijamii, shuguli hizi zinaweza kuwa kujenga jengo la serikari, viwanja vya michezo n.k. Kwa mujibu wa sheria hiyo kila mtu anahusika na shughuli hizi, mwenyeji au mgeni katika nchi hiyo ilimradi siku ya jumamosi imemkuta chini humo hanabudi kujumuika na wenyeji katika shughuli za kijamii. Kwa hiyo kulingana na utaratibu huu nasi pia ilitulazimu kuacha shughuli zetu za kongamano na kujumuika na wenyeji katika kufanya shughuli za kijamii kwa muda wa saa mbili, kuanzia saa mbili hadi saa nne.
Tulikusanyika katika jengo la gavana wa jimbo la Ngozi, akazungumza nasi, na pia alifurahia ujio wetu katika shughuli za siku ile. Baada ya maneno machache kutoka kwa Gavana tulianza kazi ya kusomba mawe kupeleka eneo lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la serikali, tulidumu kufanya kazi hiyo kwa muda wa saa mbili. Hata hivyo Gavana wa jimbo aliahidi kuliita jengo hilo kwa jina la “Jengo la vijana wa Afrika Mashariki” pindi litakapokamilika kama kumbukumbu ya wanafunzi wanaosoma kiswahili katika vyuo vikuu Afrika Mashariki.
Baada ya shughuli hizo tulirudi ukumbini kwa ajili ya mkutano mkuu wa kuchagua viongozi wapya na kufunga rasmi kongamano la 8. Na huo ndio ukawa mwisho wa kongamano la nane na pia ukawa mwanzo wa maandalizi ya kongamano la 9 ambalo litafanyika mwakani katika jiji la Kigali, Rwanda.    

Tulichojifunza juu ya Kiswahili nchini Burundi                   

Kama inavyojulikana lugha ya taifa nchini Burundi ni Kirundi na ndio lugha pekee ya asili inayozungumzwa na watu wote kutoka katika kila kona ya nchi hiyo, kwa hiyo lugha inayozungumzwa sana nchini Burundi ni Kirundi. Kutokana na ukweli huu lugha ya kiswahili nchini Burundi haijakita mizizi sana kimatumizi na hata kitaaluma. Sio kwamba kiswahili hakipo Burundi, la! Kipo lakini katika maeneo machache sana ya nchi hiyo, kwa mfano ukiwa mjini Bujumbura ndio utaweza kusikia watu wanazungumza kiswahili na pia unaweza kuwasiliana nao kwa kiswahili bila tatizo lolote, lakini hali ni tofauti katika maeneo mengine ya nchi, kwa mfano tulipokuwa katika mji wa Ngozi, tulipata shida kidogo kuwasiliana na watu hasa tulipokuwa tunajaribu kuuliza juu ya kitu fulani au tulipokuwa tunataka kununua kitu dukani, wengi walikuwa hawawezi kuzungumza kiswahili lakini pia walikuwepo baadhi waliokuwa wakizungumza kiswahili japo kwa taabu lakini ilikuwa inatosha katika kukamilisha mawasiliano.
Licha ya hali hii ya kiswahili nchini Burundi, watu wanaonesha shauku kubwa sana ya kufahamu kiswahili, kukizungumza na pia kukieneza nchini kwao. Kwa mfano chama cha kiswahili cha Burundi kinachojulikana kwa kifupi kama SAPROSS kinahusika sana na uenezaji wa kiswahili nchini humo.
Sauala jingine tulilojifunza kuhusu Kiswahili nchini Burundi ni kuhusiana na dhana potofu walionayo warundi kuhusu kiswahili. Kwa mtu anayezungumza kiswahili nchini Burundi huyo watamwona kuwa ni jambazi, mwizi, mwongo, sio mcha Mungu, muhuni na mtu asiye na maadili katika jamii. Hizi ndizo dhana zinazotawala katika vichwa vya warundi na kwa sababu hii watu wengi wamekosa msukumo wa kujifunza kiswahili kwa kuogopa kuonekana vibaya miongoni mwa jamii yao.
Pia kitu kingine tulichojifunza ni kuhusu ufundishaji wa kiswahili nchini Burundi. Ufundishaji wa kiswahili nchini Burundi ulianza miaka ya 80 katika Chuo kikuu cha Burundi, katika kitivo cha sanaa, lakini pia taasisi mbalimbali za mawasiliano zinafundisha kiswahili hasa kwa waandishi wa habari. Katika shule za msingi na sekondari kiswahili bado hakijatiliwa maanani ingawa serikali ina mpango wa kuanza kufundisha kiswahili kuanzia shule za msingi, msukumo huu umetokana na nchi hii kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika vyuo vikuu kuna walimu wanaofundisha kiswahili, walimu hawa ni wazawa wa nchi hiyo na wana mapenzi ya dhati ya kufundisha kiswahili licha ya changamoto kadha wa kadha zinazowakabili. Baadhi ya vyuo vinavyofundisha kiswahili nchini Burundi ni Chuo kikuu cha Burundi, Chuo kikuu cha Ngozi na Chuo cha Walimu, pia tulishuhudia baadhi ya walimu kutoka katika vyuo hivi wakiwasilisha makala zao ambazo kwa kweli ziliwavutia watu wengi kwa  kiswahili safi.
Licha ya kiswahili kufundishwa katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Burundi bado kuna changamoto hasa katika ufundishaji. Ufundishaji wake sio mzuri kwa mujibu wa walimu hao, kwani moja ya changamoto ni ugumu wa upatikanaji wa vitabu vya kufundishia na pia kujifunzia. Walimu na wanafunzi wa kiswahili wa Burundi wote wanakabiliwa na changamoto hii kwani upatikanaji wa vitabu vya kiswahili nchini Burundi ni mgumu sana na macho yao huelekeza Tanzania wakiamini kuwa ndio sehemu pekee kunakopikwa kiswahili na kwa hiyo hata vitabu wanavyohitaji ni kutoka Tanzania.

  Hitimisho

Ripoti hii kwa ujumla imeelezea chama cha wanafunzi wa kiswahili vyuo vikuu Afrika Mashariki na malengo ya chama hicho ambapo lengo kuu la chama hiki ni kueneza na kukienzi kiswahili. Pia katika ripoti hii tumeona hali halisi ya kiswahili Burundi.
Kwa kweli kuna juhudi zinazohitajika katika kukuza na kueneza kiswahili ndani ya Afrika Mashariki na nje kwa ujumla. CHAWAKAMA inajitahidi kulifanya hili lakini pia juhudi za ziada zinahitajika kutoka kwa wadau mabalimbali wanaojihusiha na kiswahili.
Kufanyika kwa kongamano hili Burundi tunaweza kusema kumetia hamasa kwa warundi kuwa na mwamko mpya juu ya kiswahili, kushiriki kwetu katika shughuli za kijamii kuliwadhihirishia Warundi kuwa waswahili (watu wanaozungomza kiswahili) sio wahuni wala majambazi. Kongamano hili lilitangazwa na vyombo vingi vya habari vya Burundi hasa redio na televisheni wakielezea kusudi letu sisi CHAWAKAMA kuwapo pale Burundi. Kwa hiyo lilikuwa ni tukio kubwa lililovuta usikivu wa watu kitaifa na ukizingatia ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kongamano la namna hii kufanyika Burundi. Kwa hiyo tunaweza kusema tuliacha mawazo mapya juu ya kiswahili miongoni mwa warundi.

Mapendekezo

Kiswahili kinahitajika Burundi, na kilio chao wanakielekeza Tanzania. Ni kweli warundi wako sahihi kuililia Tanzania katika kusaidia jitihada za warundi kukuza na kueneza kiswahili nchini mwao, Tanzania ndiko kunapatikana taasisi kubwa za kiswahili katika eneo lote hili la Afrika mashariki. BAKITA na TATAKI ndio taasisi zinazoangaliwa sana kama wadau wa kukuza kiswahili nchini na nje ya nchi. Kwa sababu hii napendekeza taasisi hizi zianagalie namana ya kusaidia ukuzaji wa kiswahili Burundi kwa kushirikiana na wataalamu wa kiswahili wa Burundi ambao kwa kweli wana shauku kubwa sana kuona kiswahili kinasikika Burundi kwa namna inavyostahili.
Kama tulivyokwishaona hapo awali kwamba moja ya changamoto inayowakabili walimu na wanafunzi wa kiswahili Burundi ni ukosefu wa vitabu, vitabu vingi wanavyotumia havikidhi haja yao na pengine havina ubora unaotakiwa, kwa mfano, tuliongea na mwanafunzi mmoja wa Burundi ambaye pia anajifunza kiswahili, alisema kuwa wanafunzi wengi wa chuo kikuu cha Burundi wanojifunza kiswahili huwa wanatumia jarida la FEMA la Tanzania katika kujifunza kiswahili na anasema jarida hili huwasaidia sana na wanafunzi hulipenda sana. Katika hali kama hii unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo vigumu kupata vitabu vya kujifunzia kiswahili kwa wanafunzi hawa.
Mwanafunzi huyu hakuishia hapo aliendelea kusema wanahitaji sana vitabu kutoka Tanzania, lakini pia alitoa tahadhali, kwamba vitabu ambavyo vinaweza kununuliwa na wanafunzi ni vya bei ya kuanzia faranga za Burundi 5000 hadi 15000 hii ni kutokana na uwezo mdogo wa kifedha walionao wanafunzi hao, zaidi ya hizo fedha huwenda wahadhiri ndio wanaoweza kukununua. Kwa hiyo ni vema wadau wa kiswahili mkachangamkia fursa hii.
Mwisho tuapenda kusema kuwa BAKITA na TATAKI ni wadau wa kiswahili ambao mnamalengo sawa na ya kwetu, tunaomba mkae karibu nasi, mtusaidie kwa hali na mali hasa wakati tunapotaka kuhudhuria kongamano kama hili lililokwisha. Maranyingi wanafunzi wanahudhuria wachache kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam kwa sababu hawapati ufadhili kutoka sehemu yoyote na kwa hiyo wanaohudhuria kule mara nyingi huwa wamejifadhili wenyewe, tofauti na vyuo vingine kama vile SAUT, MAKUMIRA, LAIKIPIA na vinginevyo wao miaka yote huwa wanaongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaohudhuria katika makongamano kwa sababu hufadhiliwa gharama zote na chuo chao. Kwa hiyo tunapokuja kuwaomba ufdhili msione kama tunawasumbua, nyie endeleeni tu kutufadhili na hata ikiwezeka mtusaidie kutafuta wafadhili.
Asante.
Ripoti hii imeandaliwa na
Aritamba MalagiraKatibu Mkuu
Zakia BushiriKatibu Msaidizi
“KISWAHILI, HAZINA YA AFRIKA KWA MAENDELEO ENDELEVU”
    

Sunday, October 28, 2012

VIONGOZI WA CHAWAKAMA 2012/13

MWENYEKITI

Eric Ndumbaro

MWENYEKITI MSAIDIZI

 
Theresia Mbogo

KATIBU

Aritamba Malagira


KATIBU MSAIDIZI

Zakia Bushiri

MWEKAHAZINA
Maria Mtui

KATIBU MWENEZI


Dezidery Kalinjuma

KATIBU MWENEZI MSAIDIZI


John Hhari

MHARIRI


Deo Boniface

MHARIRI MSAIDIZI
Busalu Ndege




Monday, September 24, 2012

KONGAMANO LA KISWAHILI-BURUNDI



 
  Jengo tulimokusanyika (Ukumbi kwa mwonekano wa nje)
Tunapenda kuwashukuru wote mliochangia kwa namna moja ama nyingine kutuwezesha sisi kufika katika kongamano. Kwa kweli kongamano lilikuwa zuri sana, tulijadili mada mbalimbali, makala mbalimbali ziliwasilishwa na zilikuwa ni za kuvutia sana. Napenda kuwaambia baadhi ya Makala mtazi pata humu ndani kwenye ukurasa wetu wa makala, pia tunatafuta namna ambavyo tutaweza kuweka makala hizi zikiwa katika faili la pdf.

   Mwanachawakama kutoka Kenya akiwasilisha Makala yake

Naweza kukuambia kuwa Kiswahili kinakuwa na kinapendwa sana. Nchini Burundi lugha ya taifa ni Kirundi lakini kuna idadi kubwa ya watu wanaozungumza kiswahili na wanakionea fahari sana. Tulipokuwa Bujumbura nilidhani huwenda tupo mji fulani tu wa Tanzania, huwezi kuamini watu wanawasiliana kwa kiswahili kama kawaida, na cha ajabu zaidi kuna mtaa mmoja unaitwa Buyenzi, ukifika huko utadhani kama uko mitaa ya Mbagala hivi kwani hutasikia watu wanazungumza lugha ya kiswahili kama kawaida hutasikia lugha yoyote isipokuwa kiswahili, kwa kweli hali hii ilinitia faraja.
Mahali tulipofayia kongamano Shule ya Don Bosco- Ngozi, Burundi
Ngoja nitumie fursa hii kuwatia hamasa wapenzi na wadau wa kiswahili, kwamba makongamano kama haya yanapofanyika ni vema ukahudhuria, si kwa wanafunzi wa kiswahili tu lakini pia mtu yeyote anaweza kuhudhuria ilmradi ana mapenzi na lugha ya kiswahili. huko unaweza kujifunza mambo mengi kuhusu lugha ya kiswahili na pia kama wewe ni mtaalamu wa kiswahili unaweza kuona fursa nzuri za ajira. Kwa mfano nchini Rwanda kiswahili kimeanza kufundishwa rasmi katika shule za sekondari na walimu wanahitajika sana hususani wanaotokea Tanzania, kwa hiyo unapohudhuria katika kongamano kama hili pia unaweza kupata ajira.
           Katikati ya Jiji la Bujumbura, Daladala zipo kazini
Wito wetu kwa wadau wote wa kiswahili, tunaomba tukipende na kukienzi kiswahili, ni raslimali nzuri inayoweza kulinufaisha taifa endapo viongozi wa taifa na watanzania kwa ujumla watafunguka kimawazo na kuliona hili. KONGAMANO LIJALO LITAFANYIKA KIGALI-RWANDA usipange kukosa. 


       Baada ya Kongamano, tupo katika moja ya fukwe za ziwa Tanganyika Jijini Bujumbura tunafurahia.