Kurasa Muhimu

Sunday, November 24, 2013

KATIBA YA CHAMA CHA WANAFUNZI WA KISWAHILI VYUO VIKUU VYA AFRIKA MASHARIKI

          KATIBA YA CHAMA
CHAMA CHA WANAFUNZI WA KISWAHILI VYUO VIKUU VYA AFRIKA MASHARIKI

YALIYOMO:

SEHEMU YA KWANZA
  • JINA LA CHAMA
  • WALEZI WA CHAMA
SEHEMU YA PILI
  • MADHUMUNI YA CHAMA
SEHEMU YA TATU
  • UANACHAMA NA ADA
  • AINA ZA UANACHAMA
  • HAKI ZA MWANACHAMA
  • KIINGILIO NA ADA YA MWAKA
  • KUSITA UANACHAMA
SEHEMU YA NNE
  • MUUNDO WA UONGOZI
  • MUDA WA UONGOZI
  • MASHARTI YA UONGOZI
  • WAJIBU WA VIONGOZI
SEHEMU YA TANO
  • FEDHA ZA CHAMA
  • VYANZO VYA MAPATO
  • UWEKAJI, UCHUKUAJI WA FEDHA
SEHEMU YA SITA
  • VIKAO VYA CHAMA
  • KAMATI KUU
  • MKUTANO MKUU WA CHAMA
SEHEMU YA SABA
  • MABADILIKO YA KATIBA



SEHEMU YA KWANZA

1.1 JINA LA CHAMA
Jina la chama litakuwa CHAMA CHA WANAFUNZI WA KISWAHILI VYUO VIKUU VYA AFRIKA MASHARIKI (kwa kifupi CHAWAKAMA)
Makao makuu ya CHAWAKAMA yatakuwa CHUO KIKUU CHA WAISLAMU MOROGORO.


1.2 WALEZI WA CHAMA
walezi wa chama watakuwa:
1.2.1Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) kutoka nchini Kenya.
1.2.2 Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) kutoka Tanzania.
1.2.3 Chama cha Kiswahili cha Uganda.

SEHEMU YA PILI

2.0 MADHUMUNI YA CHAMA
2.1 Kuwapa wanachama nafasi ya kujadili, kuimarisha na kuendeleza vipawa vyao vya lugha na fasihi ya Kiswahili
2.2 Kuamsha ari ya mapinduzi ya utamaduni wa lugha ya Kiswahili
2.3 Kueneza lugha ya kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki
2.4 Kushirikiana na vyama vingine vya Kiswahili katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki.
2.5 Kuunganisha wanafunzi wa lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki
2.6 Kushirikiana na Asasi mbalimbali zinazojihusisha na ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili Afrika Mashariki na Afrika yote kwa ujumla
2.7 Kuratibu makongamano ya mijadala mbalimbali.
2.8 Kuchapisha kijarida cha CHAWAKAMA na machapisho mengine ili kukuza taaluma ya kiswahili.
2.9 Kubuni mikakati na mbinu za kuhimiza ukuzaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili.
2.10 Kuweka kumbukumbu ya wataalamu kwa nia ya kuwatumia katika kufanikisha malengo ya chama na wahusika wa Kiswahili kwa ujumla.

SEHEMU YA TATU 

3. UANACHAMA NA ADA
Yupo huru mtu yeyote anayependa kujiunga na kutekeleza mambo yote yanayohusiana na chama kama kulipa kiingilio na ada, kuhudhuria vikao na kushiriki katika kuiendeleza lugha ya kiswahili.

3.1 AINA ZA UANACHAMA

3.1.1 Uanachama wa kawaida
3.1.1.1 Wanachama walio chuoni
unawahusu wanafunzi wote wanaosoma somo la kiswahili katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki katika kiwango cha shahada ya kwanza na shahada za Uzamili na Uzamivu.
3.1.1.2 Wanachama nje ya Chuo
Unawahusu wote walio nje ya chuo na waliohitimu masomo wakiwa wanachama wa CHAWAKAMA:
Iwapo ataomba uanachama kwa kujaza fomu maalumu.

3.1.2 Wanachama Washiriki
Asasi zinazoshughulikia ukuzaji na uenezaji wa Kiswahili zinaweza kukubaliwa kuwa mwanachama baada ya kuwasilisha maombi na kukubaliwa na kamati ya utendaji ya chama kwa kutimiza masharti yatakayotolewa.

3.1.3 Uanachama wa Heshima
Hawa ni watu/taasisi ambazo kwa mchango maalumu wameonekana/zimeonekana zinafaa kupewa uanachama wa heshima.

 3.1.4 Uanachama wa Wadhifa
Unawahusu walezi na wanataalama wa somo la kiswahili.

3.1.5 Haki za mwanachama
Wanachama wote isipokuwa wanachama washiriki, wanachama wa heshima na wanachama wa wadhifa watakuwa na haki zifuatazo:
3.1.5.1 Kupiga kura wakati wa uchaguzi
3.1.5.2 kugombea uongozi katika chama kwa mujibu wa katiba hii.
3.1.5.3 Kuwasilisha hoja kwa ajili ya kujadiliwa katika mkutano mkuu.

3.3 KIINGILIO NA ADA YA MWAKA
3.3.1 Kila mwanachama atalipa kiingilio ambacho kitapangwa na kamati ya utendaji na kuthibitishwa na mkutano mkuu.
3.3.2 Kila mwanachama atatakiwa kutoa ada ya mwaka, kiasi ambacho kitapangwa na kamati ya utendaji na kuthibitishwa na mkutano mkuu.
3.3.3 kila mwanachama mpya aliyejiunga kwa mara ya kwanza atalipa Sh. 10,000/= na yule wa zamani atalipa Sh. 8,000/=

3.3.4. Fedha zote katia kipengele (c) hapo juu zitakuwa katika mgawanyo ufuatao;
        3.3.4.1. Sh. 2000/= kwa ajili ya kitambulisho (kwa mwanachama mpya)
        3.3.4.2  Asilimia 30 itakwenda Afrika Mashariki, Asilimia 30 nyingine itakwenda kanda na Asilimia 40 itabaki tawini.Viwango hivi vitakuwa vikibadilika kulingana na wakati.

3.4 KUSITA UANACHAMA.
Uanachama utasita kwa sababu zifuatazo:
3.4.1 Kutohudhuria mkutano wa chama mara tatu mfululizo bila ya taarifa na sababu za kuridhisha.
3.4.2 Kutolipa ada ya mwaka kwa muda wa miaka miwili mfululizo.
3.4.3 kujiuzulu uanachama
3.4.4 Kufukuzwa au kuachishwa uanachama na mkutano mkuu kwa kura zisizopungua robo tatu ya wajumbe waliohudhuria.
3.4.5 Kifo cha mwanachama
3.4.6 Kutokuwa katika hali ya akili timamu.

SEHEMU YA NNE

4.1 MUUNDO WA UONGOZI
4.1.1Kutakuwa na uongozi wa kanda.Kanda ya Tanzania, Kanda ya Kenya, Kanda ya Uganda, Kanda ya Rwanda, Kanda ya Burundi na Uongozi wa Makao Makuu Afrika Mashariki
4.1.2 Viongozi wa CHAWAKAMA katika kanda watakuwa: Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti, Katibu Mkuu, Naibu Katibu, Mweka Hazina, Mweka hazina Msaidizi, Afisa Uhusiano, Afisa Uenezi, Mhariri Mkuu, Mhariri Msaidizi.
4.1.3 Viongozi CHAWAKAMA Afrika Mashariki watakuwa: Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mweka Hazina, Mweka Hazina Msaidizi, Afisa Uhusiano, Afisa Uenezi, Mhariri Mkuu, Mhariri Msaidizi na Mjumbe mmoja kutoka kila kanda (nchi)
4.1.4 Viongozi wa CHAWAKAMA kanda na wa Afrika Mashariki watachaguliwa na mkutano mkuu.
4.1.5 Kwa kadri inavyowezekana nafasi za uongozi wa Chama zitagawanywa sawa kwa nchi wanachama kwa upande wa Afrika Mashariki na kwa matawi husika katika kila kanda isipokuwa Katibu Mkuu atatoka Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro kwa sababu za kiutendaji kwa vile ndipo Makao Makuu ya kudumu ya CHAWAKAMA yalipo.
4.1.6 Viongozi hao pamoja na wawakilishi wawili kutoka kila nchi, yaani Mwenyekiti na Katibu wa tawi wa nchi husika, wataunda kamati ya utendaji.

4.2 MUDA WA UONGOZI
kamati ya utendaji itakuwa madarakani kwa muda wa mwaka mmoja. Wajumbe wa kamati wanaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi kingine kisichozidi miaka miwili isipokuwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Mhazini ambao wataongoza kwa mwaka mmoja tu na nafasi zao kupokelewa na makamu au manaibu wao.

4.3 MASHARTI YA VIONGOZI
Kiongozi anatakiwa:
a) Kuwajibika kwa mujibu wa katiba 
b) Kuhudhuria vikao vyote vya Chama
c) Kutunza mali na hadhi ya Chama
d) Kutokuwa mla wala mtoa rushwa
e) Kujiuzulu anapoona kazi imemshinda
f) Kukubali kuwajibika.

4.4 WAJIBU WA VIONGOZI
4.4.1 Mwenyekiti wa Kanda
Atafanya kazi zifuatazo katika ngazi ya kanda
  • Msimamizi mkuu wa shughuli za Chama
  • Msemaji mkuu wa Chama
  • Mwongoza mikutano ya Chama (kamati kuu na mkutano mkuu)
  • Kiongozi wa misafara ya Chama
  • Kusimamia nidhamu ya viongozi 
4.4.2 Makamu wa Mwenyekiti Kanda
  • Msaidizi mkuu wa Mwenyekiti
  • Mwenyekiti wa vikao vyote vya Chama kama Mwenyekiti hayupo.
  • Msaidizi na Mshauri wa Mwenyekiti
  • Kufanya kazi nyingine atakazo agizwa na mwenyekiti.
4.4.3 Katibu Mkuu Kanda
  • Mtendaji Mkuu wa Chama
  • Mtunza kumbukumbu za Chama
  • Mtunza mali ya Chama
  • Katibu wa mikutano ya Chama
  • Kuitisha vikao
  • Kuidhinisha matumizi ya fedha za Chama
  • Kuratibu shughuli za Chama
  • Kutoa ripoti juu ya maendeleo ya Chama
  • Kutunza orodha ya Wanachama
  • Kutunza mihuri ya Chama
4.4.4 Katibu Msaidizi Kanda
  • Msaidizi wa Katibu Mkuu
  • Mshauri wa Katibu Mkuu
  • Kufanya kazi zote za katibu Mkuu endapo kama hayupo
  • Kufanya kazi nyingine atakazoagizwa na Katibu Mkuu.
4.4.5 Mweka Hazina Kanda
  • Atakuwa mdhibiti mkuu wa fedha na mali za Chama.
  • Atahakikisha kuwa kuna mfumo mzuri wa kupokea, kudhibiti na kulipa fedha za Chama.
  • Atatengeneza makisio ya mapato na matumizi ya Chama.
  • Atafanya malipo kwa kufuata taratibu na kanuni za fedha zilizowekwa
  • Atakuwa mweka saini wa lazima katika akaunti za benki za Chama
  • Ataandika na kutunza vitabu vya hesabu ya Chama
  • Atatayarisha hesabu na taarifa za fedha za mwaka na kuziwasilisha kwa kamati ya utendaji kabla ya kuwasilisha katika Mkutano Mkuu
  • Atatunza na kudhibiti rasilimali za Chama
  • Atahakikisha kuwa kila mwisho wa mwaka wa fedha, mali yote inahakikiwa.
4.4.6 Mweka hazina Msaidizi
  • Atamsaidia mweka hazina kudhibiti fedha na mali za Chama
  • Kusaidia kuhakikisha kuwa kuna mfumo mzuri wa kupokea, kudhibiti na kulipa fedha za Chama.
  • Kusaidia kufanya malipo kwa kufuata taratibu na kanuni za fedha zilizowekwa
  • kusaidia kutengeneza makisio ya mapato na matumizi ya Chama
  • Atafanya kazi zote atakazoagizwa na Mweka hazina mkuu pamoja na Mwenyekiti
4.4.7 Afisa Uhusiano Kanda
  • Atabuni na kuratibu mipango ya ushirikiano miongoni mwa nchi na asasi wanachama
  • Kutembelea asasi wanachama ili kufuatilia shughuli za Chama
  • Katika utekelezaji wa majukumu haya, Afisa uhusiano atashirikiana kwa karibu na Katibu na Makamu Mwenyekiti, Naibu Katibu, na Mhariri Mkuu.
4.4.8 Afisa Mwenezi Kanda 
  • Atasimamia utangazaji na uenezi wa shughuli za Chama ili kuleta mahusiano mema na maelewano na umma, Vyombo vya Habari, Serikali, Mashiirika ya Uhisani na asasi nyinginezo.
4.4.9 Mhariri Mkuu Kanda
  • Atasimamia na kuratibu uandaaji, uhariri na utoaji wa jarida la Chama pamoja na vitabu . Machapisho hayo yanaweza kuwa katika umbo la karatasi au la elektroniki.
  • Atakuwa ndiye mratibu mkuu wa masuala ya ushirikiano katika uchapishaji na ubadilishaji wa machapisho.
4.4.10 Mhariri Msaidizi Kanda
  • Atasaidiana na mhariri mkuu katika kufanikisha majukumu ya uhariri katika chama
4.5.1 Mwenyekiti wa Afrika Mashariki
Atatekeleza majukumu au kazi zifuatazo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Msimamizi mkuu wa shughuli za Chama
  • Msemaji mkuu wa Chama
  • Mwongoza mikutano ya Chama (kamati kuu na mkutano mkuu)
  • Kiongozi wa misafara ya Chama
  • Kuidhinisha kusitisha uanachama
  • Kusimamia nidhamu ya viongozi
4.5.2 Makamu wa mwenyekiti wa Afrika Mashariki
Atatekeleza kazi zifuatazo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Msaidizi mkuu wa Mwenyekiti
  • Mwenyekiti wa vikao vyote vya Chama kama mwenyekiti hayupo
  • Msaidizi na mshauri wa Mwenyekiti
  • Kufanya kazi nyingine atakazoagizwa na Mwenyekiti
4.5.3 Katibu Mkuu Afrika Mashariki
Atatekeleza kazi zifuatazo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Mtendaji mkuu wa Chama
  • Mtunza kumbkumbu za Chama
  • Mtunza mali za Chama
  • Katibu wa mikutano ya Chama 
  • Kuitisha vikao
  • Kuidhinisha matumizi ya fedha za chama
  • Kuratibu shughuli za Chama
  • Kutoa ripoti juu ya maendeleo ya Chama
  • Kutunza orodha ya wanachama
  • Kutunza mihuri ya Chama
4.5.4 Katibu Mkuu Msaidizi Afrika Mashariki
Atatekeleza kazi au wajibu zifuatazo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Msaidizi wa Katibu Mkuu
  • Mshauri wa katibu
  • Kufanya kazi zote za Katibu Mkuu wakati hayupo
  • Kufanya kazi nyingine atakazoagizwa na Katibu Mkuu
4.5.5 Mweka Hazina Afrika Mashariki
Atakuwa na majukumu yafuatayo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Atakuwa mdhibiti mkuu wa fedha na mali za Chama
  • Atahakikisha kuwa kuna mfumo mzuri wa kupokea, kudhibiti na kulipa fedha za Chama
  • Atatengeneza makisio ya mapato na matumizi ya Chama
  • Atafanya malipo kwa kufuata kanuni za fedha zilizowekwa
  • Atakuwa mweka saini wa lazima katika akaunti za benki za Chama
  • Ataandika na kutunza vitabu vya hesabu ya Chama
  • Ataandaa hesabu na taarifa za fedha za nwaka na kuziwasilisha kwa kamati ya utendaji kabla ya mkutano mkuu
  • Atatunza na kudhibiti mali na rasilimali za Chama
  • Atahakikisha kwamba kila mwisho wa mwaka wa fedha, mali inahakikiwa.
4.5.6 Mweka Hazina Msaidizi Afrika Mashariki
Atatekeleza majukumu yafuatayo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Atamsaidia mweka hazina kudhibiti fedha na mali za Chama
  • Kusaidia kuhakikisha kuwa kuna mfumo mzuri wa kupokea, kudhibiti na kulipa fedha za Chama
  • Kusaidia kutengeneza makisio ya mapato na matumizi ya Chama
  • Kusaidia kufanya malipo kwa kufuata taratibu na kanuni za fedha zilizowekwa
  • Atafanya kazi zote atakazoagizwa na mweka Hazina Mkuu pamoja na Mwenyekiti
4.5.7 Afisa Uhusiano Afrika Mashariki
Atatekeleza majukumu yafuatayo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Atabuni na kuratibu mipango ya uhusiano miongoni mwa nchi na asasi Wanachama
  • Kutembelea asasi wanachama ili kufuatilia shughuli za Chama
  • Katika utekelezaji wa majukumu haya, Afisa ushirikiano atashirikiana kwa karibu na Katibbu na Makamu Mwenyekiti, Naibu Katibu na Mhariri Mkuu.
4.5.8 Afisa Mwenezi Afrika Mashariki
Atatekeleza majukumu yafuatayo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Atasimamia utangazaji na uenezi wa shughuli za Chama ili kuleta mahusiano meme na maelewano na uma, vyombo vya habari, serikali, mashirika ya uhisani na asasi nyinginezo
4.5.9 Mhariri Mkuu Afrika Mashariki
Atatekeleza majukumu yafuatayo katika ngazi ya Afrika Mashariki:
  • Atasimamia na kuratibu uandaaji. uhariri na utoaji wa jarida la Chama pamoja na vitabu. Machapisho hayo yanaweza kuwa katika umbo la karatasi au la kielektroniki
  • Atakuwa ndiye mratibu mkuu wa masuala ya ushirikiano katika uchapishaji na ubadilishaji wa machapisho.
4.5.10 Mjumbe kutoka kila nchi Afrika Mashariki
Atatekeleza majukumu yafuatayo katika ngazi ya Afrika Mashariki
  • Atakuwa ni mwakilishi kutoka kwenye nchi yake.Akisaidiana na uongozi, Atakuwa akifanya shughuli za za chama katika nchi yake; atakuwa mwenyeji wa uongozi wa ngazi za juu utakapotembelea nchi yake.
SEHEMU YA TANO

5.0 FEDHA ZA CHAMA
5.1 Vyanzo vya mapato
Mapato ya Chama yatatokana na:
5.1.1Kiingilio na ada ya kila mwaka ya mwanachama
5.1.2 Misaada, Zawadi au ruzuku kutoka kwa wafaadhili, wanachama, wahisani, watu binafsi na vyombo vingine
5.1.3 Mapato yatokanayo na shughuli mbalimbali au miradi ya Chama
5.1.4 Fedha itokanayo na mikopo
5.1.5 Mwanachama au mfadhili yeyote wa chama anaweza kutoa fedha kukisaidia Chama kwa njia yoyote atakayoona inafaa.

5.2 Uwekaji, Uchukuaji wa fedha
5.2.1 Uwekaji wa fedha
Fedha za chama zitahifadhiwa atika benki itakayoteuliwa na kamati tendaji

5.2.2 Kutafunguliwa akaunti mbili katika benki:
5.2.2.1 Akaunti ya matumizi ya kawaida
5.2.2.2 Akaunti ya mfuko wa maendeleo wa ukuzaji na uenezaji wa lugha

5.2.3 Watia Saini
5.2.3.1 Mwenyekiti
5.2.3.2 Katibu
5.2.3.3 Mhazini
             Kamati kuu itaandaa utaratibu wa kuchukua fedha hizo benki.

SEHEMU YA SITA

6.0 VIKAO VYA CHAMA
6.1 Kamati kuu
6.1.1 Wajumbe wa kamati kuu
      Viongozi wote waliochaguliwa na mkutano mkuu.
6.1.2 Akidi: Nusu ya wajumbe wote

6.2 Kazi za Kamati Kuu
6.2.1 Kutafuta vyanzo vya mapato
6.2.2 Kutengeneza na kuratibu sera za Chama
6.2.3 Kuandaa programu ya shughuli za Chama
6.2.4 Kuangalia maendeleo ya Chama
6.2.5 Kusimamia shughuli za Chama
6.2.6 Kutoa mapendekezo ya Chama na kusimamia utekelezaji wake
6.2.7 Kuunda kamati mbalimbali za utendaji kutegemeana na uhitaji 
6.2.8 Kusimamia ajenda za mkutano mkuu.

6.3 Idadi ya vikao vya kamati kuu vitafanyika mara mbili kwa mwaka. Aidha vikao vya dharura vitakuwepo endapo vitahitajika

6.4 Mkutano Mkuu wa Chama
6.4.1 Wajumbe wa Mkutano Mkuu
Ni wanachama wote
6.4.2 Akidi: Theluthi moja (1/3) ya wanachama wote
6.4.3 Kazi za Mkutano Mkuu
  • Kuchagua viongozi
  • Kupitisha mapendekezo ya kamati
  • Kupokea taarifa ya kamati
  • Kutoa ushauri katika uendeshaji wa Chama
6.5 Idadi ya vikao vya Mkutano Mkuu
Mkutano Mkuu utafanyika mara moja kwa mwaka na vikao vya dharura vitafanyika iwapo vitahitajika.

SEHEMU YA SABA

7.0 Mabadiliko ya Katiba
Katiba hii inaweza kubadilishwa, kuhuishwa au kurekebishwa na Mkutano Mkuu wa chama ulioitishwa kwa madhumuni hayo na kupitishwa kwa theluthi mbili.













Friday, November 22, 2013

                         WANACHAMA, WADAU NA MASHABIKI WA BLOGI HII BILA SHAKA MNAENDELEA VYEMA NA MAJUKUMU YENU YA KILA SIKU IKIWA NI PAMOJA NA KUKIENZI KISWAHILI KAMA TUNU NA AMALI YA AFRIKA.
      
      Chuo kikuu cha Dar es Salaam kimepata bahati ya kutembelewa na nguli mtetezi wa lugha za Afrika, Prof. Ngugi wa Thiong'o Tar. 22 Novemba, 2013 ambapo alikuwa na kongamano na wanafunzi hapa chuoni katika ukumbi wa Nkurumah.
      Katika kongamano hilo Profesa Ngugi alisizitiza suala la lugha kuwa ni silaha ya kivita kwa jamii yoyote ile dhidi ya harakati za kuleta umoja na maendeleo, hivyo akawaasa wanazuoni na waafrika kuzitukuza na kuziendeleza lugha zetu ikiwa ni pamoja na kuikuza lugha ya Kiswahili ili iweze kuwa miongoni mwa lugha kubwa duniani kama ilivyo kwa lugha ya kiingereza, kifaransa kiarabu na nyingine kama hizo.
      Moja ya mifano yake ni pamoja na kuwaonya wanazuoni kutofanana na majemadari wa kivita ambao wametekwa na maadui huku raia wakitegemea ushindi kutoka kwao, kwani kutumia lugha za kigeni mfano kiingereza ambacho kinatumiwa na mabepari kama silaha ya kututawala, kama lugha ya kufundishia ili hali tuna lugha zetu za asili ya kiafrika, huku tukitegemea kuleta umoja na mshikamano ni kujidanganya na kamwe hatutoshinda kwani tunajenga tabaka la waliosoma yaani wanaojua kiingereza na wale wasio soma yaani wasiojua kiingereza. Je mlio wasomi mtafikishaje maarifa yenu kwa wale ambao hawakubahatika kuipata elimu hasa ya ngazi za juu?, kwa lugha ya kiingereza?, Na baada ya kuhitimu mnaenda kuhudumia jamii lugha ya aina gani?, ya wanaozungumza kiingereza?, Jibu kila mdau analo. Chondechonde ewe mzalendo chukua hatua madhubuti kuiokoa Afrika katika mateka hii ya lugha.
       Profesa Ngugi anatuhasa kuzitumia lugha zetu za kiafrika hasa lugha ya Kiswahili katika kutolea elimu na nyanja nyingine ili kufanikisha azma ya waasisi wetu kama Mwalimu J.K Nyerere, na Nkurumah ambao walikua na dhamira ya kuifanya Afrika iwe na lugha moja. kuhusu lugha za kigeni alisema zitumike kuongeza maarifa zaidi na maarifa hayo tuyatafsiri katika lugha yetu tukufu ili kila mzawa wa bara hili aweza kufaidika.
       kwa ufupi hayo ndiyo yaliyojiri katika kongamano hilo ambalo lilihudhuriwa na makamu mkuu wa chuo Profesa R. Mkandala,Timu ya wataalamu wa lugha toka TATAKI ikiongozwa na Prof. M.M. Mlokozi, Maprofesa kutoka vitivo na shule ndani ya chuo, madaktari,wahadhiri wakufunzi, na wadau mbalimbali wa lugha na fasihi pamoja na wanafunzi.  
                Kwa maoni, ushauri, pendekezo au swali kuhusu mawazo haya ya profesa Ngugi wa Thion'go usisite kuyatoa kwetu. ahsante. 
                                      Imeandaliwa na kuwasiliswa kwenu na,
                                                 mhariri mkuu
                                                         CHAWAKAMA CKD,
                                                                        Athanas Barnabas.   

Tuesday, May 7, 2013

VIONGOZI WA CHAWAKAMA 2013/2014

                                              VIONGOZI WA CHAWAKAMA 2013/2014
Mwenyekiti Fina Munish, Mwenyekiti msaidizi Ilomo Stainley, Katibu mkuu Abel Patrick, katibu msaidizi kibasu mwanzani, katibu mwenezi Lucas Philemon, Katibu mwenezi msaidizi Mwilolezi Judith, Mhariri Athanas Barnaba, Mhariri msaidizi Lyimo Emannuel, mhazini Kagwa Phidesi Mwakilishi TATAKI Masija Nyasatu, Mwakilishi BAED Mgata 

                                           VIONGOZI WA CHAWAKAMA KWA UJUMLA
                                                             MWENYEKITI

                                                              FINA  MUNISHI

                                                          MWENYEKITI MSAIDIZI
                                                           ILOMO STANLEY       
                                                           
                                                                      KATIBU MKUU
                                                               ABEL PATRICK

Thursday, January 10, 2013

RIPOTI YA KONGAMANO LA 6 CHAWAKAMA KANDA YA TANZANIA LILILOFANYIKA MUCE-IRNGA



Shukrani
Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa wale wote walioshirikiana nasi hadi kufanikisha kuhudhuria kongamano hili. Kwa kweli ilikuwa ni changamoto kubwa kufanikisha kuhudhuria katika kongamano kutokana na uhaba wa pesa tulio nao. Pamoja na changamoto hizo lakini uongizi wa chawakama ulithubutu kumpeleka kiongozi mmoja ili kuwakilisha tawi letu, tunawashukuru sana.
Vilevile tunawashukuru sana wanachama waliojinyima na kuamua kutumia pesa kwenda MUCE ili kuwakilisha tawi letu, mmetujengea heshima kubwa, tunawashukuru sana.
Mwisho kabisa tunapenda kumshukuru Katibu msaidizi kwa moyo wake wa kujitolea, kutokana na ukata unaoukabili CHAMA, aliamua kutumia pesa zake ili kufanikisha kuhudhuria katika kongamano.
Utangulizi
CHAWAKAMA-UDSM imekuwa mstari wa mbele katika kuhakisha malengo ya chama yanasonga mbele. Uwakilishi wetu katika makongamano umekuwa ni mzuri sana. Tangu kongamano la kwanza (1) la kanda hadi hili la sita (6) tumekuwa na uwakilishi katika kila kongamano, japokuwa idadi ya wawakilishi inakuwa ndogo lakini angalau tunakuwa na uwakilishi.
Kwa kuzingatia mlolongo huu wa kuandaa makongamano, kongamano la 6 limefanyika katika Chuo Kikuu kishiriki Cha Mkwawa (MUCE). Kama ilivyokawaida yetu sisi CHAWAKAMA-UDSM katika kutimiza majukumu muhimu ya chama, tulituma uwakilishi katika kongamano hili. Jumla ya washiriki kutoka tawi letu waliohudhuria ni wanne (4). Kiongozi mmoja na wanachama wa kawaida watatu. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanachama zaidi ya 100 tulionao lakini sababu pekee ya idadi hii ni kutokana na uhaba wa pesa tulionao.
Kwa hiyo ripoti hii ina lenga kuelezea kile kilichojiri katika kongamano la 6 lililofanyika MUCE-Iringa.
KONGAMANO LENYEWE
Kongamano la 6 la kitaifa la CHAWAKAMA mwaka 2013 lilifanyika katika chuo kikuu kishiriki cha Mkwawa (MUCE) – Iringa. MUCE ndio walio kuwa wenyeji wa kongamano la 6 mwaka 2013.
Washiriki kutoka vyuo mbalimbali vya Tanzania walihudhuria ikiwa ni pamoja na washiriki kutoka shule ya Sekondari Mlamke. Washiriki wa kongamano walianza kuwasili tarehe 20 Feburuari kutoka katika vyuo mbalimbali kutoka maeneo tofautitofauti ya Tanzania. Miongoni mwa vyuo hivyo Chuo kikuu cha Dar es Salaam hakikuwa nyuma na kiliwakilishwa na wanachama wanne. Baada ya kuwasili tulikaribishwa kwa bashasha na wenyeji wetu na siku hiyo ilikuwa ni siku ya maadalizi kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa kongamano.
Tarehe 21 Feburuari ndio ilikuwa siku rasmi ya ufunguzi wa kongamano. Kabla ya kuingia ukumbini asubuhi ya siku hiyo kwa ajili ya ufunguzi rasmi tulifanya maandamano kwa kuimba nyimbo za kukitukuza Chama chetu. Baada ya kuingia ukumbini tuliketi chini na kumsikiliza Manju ili kujua kile kilichokuwa kinafuata kwa mujibu wa ratiba ya siku hiyo.
Ilipotimia saa 3 asubuhi kongamano lilifunguliwa rasmi. Mgeni rasmi wa kongamano alikuwa ni Makamu Meya (Deputy Mayor) wa Manispaa ya Iringa Ndugu Gervance Ndaki ambaye alikuja kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa.
Baada ya ufunguzi huo ilifuata risala iliyosomwa na Mwenyekita wa Kanda ya Tanzania kwa mgeni rasmi. Risala hiyo ilihusu maendeleo ya chama kwa ujumla ambayo ni mazuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo Kiswahili hakikuwa na hadhi ya juu ukilinganisha na sasa ambapo tunaona Kiswahili kimenea na kukua kwa kasi sana. Pamoja na mafanikio hayo pia risala ilionesha jinsi chama kinavyokabiliwa na changamoto. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa fedha kwa ajili ya kuendeshea chama, kwa mfano kushindwa kuandaa makongamano kwa fedha za chama na badala yake tunategemea malipo yanayofanywa na wanachama, hii inamaana kwamba bila wanachama kuchangia hatuwezi kuandaa kongamano. Pia kutokana na uhaba wa fedha chama kimeshindwa kusajiliwa mpaka hivi sasa kitu ambacho ni tatizo kubwa kwa kutotambulika kwa chama chetu kisheria.