Kurasa Muhimu

Monday, September 24, 2012

KONGAMANO LA KISWAHILI-BURUNDI



 
  Jengo tulimokusanyika (Ukumbi kwa mwonekano wa nje)
Tunapenda kuwashukuru wote mliochangia kwa namna moja ama nyingine kutuwezesha sisi kufika katika kongamano. Kwa kweli kongamano lilikuwa zuri sana, tulijadili mada mbalimbali, makala mbalimbali ziliwasilishwa na zilikuwa ni za kuvutia sana. Napenda kuwaambia baadhi ya Makala mtazi pata humu ndani kwenye ukurasa wetu wa makala, pia tunatafuta namna ambavyo tutaweza kuweka makala hizi zikiwa katika faili la pdf.

   Mwanachawakama kutoka Kenya akiwasilisha Makala yake

Naweza kukuambia kuwa Kiswahili kinakuwa na kinapendwa sana. Nchini Burundi lugha ya taifa ni Kirundi lakini kuna idadi kubwa ya watu wanaozungumza kiswahili na wanakionea fahari sana. Tulipokuwa Bujumbura nilidhani huwenda tupo mji fulani tu wa Tanzania, huwezi kuamini watu wanawasiliana kwa kiswahili kama kawaida, na cha ajabu zaidi kuna mtaa mmoja unaitwa Buyenzi, ukifika huko utadhani kama uko mitaa ya Mbagala hivi kwani hutasikia watu wanazungumza lugha ya kiswahili kama kawaida hutasikia lugha yoyote isipokuwa kiswahili, kwa kweli hali hii ilinitia faraja.
Mahali tulipofayia kongamano Shule ya Don Bosco- Ngozi, Burundi
Ngoja nitumie fursa hii kuwatia hamasa wapenzi na wadau wa kiswahili, kwamba makongamano kama haya yanapofanyika ni vema ukahudhuria, si kwa wanafunzi wa kiswahili tu lakini pia mtu yeyote anaweza kuhudhuria ilmradi ana mapenzi na lugha ya kiswahili. huko unaweza kujifunza mambo mengi kuhusu lugha ya kiswahili na pia kama wewe ni mtaalamu wa kiswahili unaweza kuona fursa nzuri za ajira. Kwa mfano nchini Rwanda kiswahili kimeanza kufundishwa rasmi katika shule za sekondari na walimu wanahitajika sana hususani wanaotokea Tanzania, kwa hiyo unapohudhuria katika kongamano kama hili pia unaweza kupata ajira.
           Katikati ya Jiji la Bujumbura, Daladala zipo kazini
Wito wetu kwa wadau wote wa kiswahili, tunaomba tukipende na kukienzi kiswahili, ni raslimali nzuri inayoweza kulinufaisha taifa endapo viongozi wa taifa na watanzania kwa ujumla watafunguka kimawazo na kuliona hili. KONGAMANO LIJALO LITAFANYIKA KIGALI-RWANDA usipange kukosa. 


       Baada ya Kongamano, tupo katika moja ya fukwe za ziwa Tanganyika Jijini Bujumbura tunafurahia.