WAPENZI NA WANADAU WA WAVUTI YETU YA CHAWAKAMA CKDSM ZAMANI CHAWAKAMA UDSM LEO TUNAWALETEA MAKALA ILIYOWASILISHWA NA WANACHAMA WETU KATIKA KONGAMANO LA KITAIFA LA CHAWAKAMA KANDA YA TANZANIA LILILOFANYIKA KATIKA CHUO CHA EKENFORDE FEBRUARI, 2014 MJINI TANGA.
MCHANGO WA SHAABAN ROBERT
KATIKA UWANJA WA FASIHI YA KISWAHILI
Pacho Peter na
Kazinja Geniva
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania
IKISIRI
Shaaban Robert katika ulimwengu wa
Fasihi ya Kiswahili ni nguli ambaye ni maarufu katika masikio ya wanazuoni na
wasomi. Kazi zake zimetanda na kutamalaki kiasi kwamba baadhi ya wasomi na
wadau wa lugha na fasihi ya Kiswahili hushawishika kumwita baba wa fasihi ya
Kiswahili. Ubaba huu wa fasihi unaifanya historia ya fasihi kumwweka nguli huyu
katika nafasi iliyotukuka na isiyo na kifani. Makala haya, yanaangazia mchango
wa nguli huyu Shaaban Robert katika Uwanja wa Fasihi ya Kiswahili.
1.0 Utangulizi
Chuachua (2011:38-40) anaeleza kuwa
jina la mwandishi
huyu limezua mitazamo
tofautitofauti kwa kuwa
limejumuisha majina mawili
yenye asili na
utamaduni tofauti. Jina
lake la kwanza
lina asili ya Uislamu
(Shaaban) na lingine
lina asili ya
Ukristu (Robert). Wapo
waliodhani kuwa amejiita
hivyo ili kuonesha
msimamo wa kati
kuhusu dini, kwa
kuwa dini zote
zina hadhi sawa.
Wengine wameeleza kuwa
jina la Robert
ni la Mwitaliano
aliyekuwa mwajiri wa
baba yake mzee
Selemani Ufukwe.
Anaendelea kueleza
kuwa jina halisi
la baba yake
Shaaban Robert ni
“Lubeti” ambalo bila
shaka ndilo lililopata
athari ya kimatamshi
na kuwa Robert.
Watu wengi wameandika
kuhusu maisha yake
lakini kwa bahati
mbaya taarifa kuhusu
maisha ya kifo
chake imekuwa ikikosewa
mara kwa mara.
Tarehe ya kuzaliwa kwake wengi
wanakubaliana kuwa ni tarehe
1.01.1909, bila shaka
hii ni tarehe
sahihi.
Anaendelea kueleza
kuwa baadhi ya
watafiti kama (Gibbe
1978, Kezilahabi 1976) wanasema
kuwa Shaaban Robert
alifariki tarehe 22.06.1962
akazikwa Machui. Aidha
utafiti wa uwandani
ulioshehenezwa maelezo ya
mwanae Ikbal inaonesha
kuwa Shaaban Robert
alifariki tarehe 20.06.1962
na kuzikwa huko
vibambani tarehe 21.06.1962.
kwa maoni ya
mtafiti anaona ni
vema kukubaliana na
maelezo ya mwanaye
kwa kuwa alishuhudia
kufa na kuzikwa
kwa baba yake.
Kabla ya kifo
chake, makazi yake
ya awali yalikuwa barabara
ya tisa, Tanga
mjini.
Anaendelea kueleza
kuwa mwandishi huyu
alianza kuandika akiwa
hakwenda mbali kielimu.
Alianza shule mwaka
1922 na kumaliza
mwaka 1926 mjini
Dar es Salaam
katika shule ya
Kichwele (Uhuru Mchanganyiko). Elimu
yake ndogo haikuwa
kikwazo, alijipambanua mapema
kama mwandishi mashuhuri.
Jitihada zake za
kufika mbali kielimu
hazikuzaa matunda kwa
haraka, ziliporwa na
wakoloni kwa lengo
la kumtumia kama
chombo cha kutawalia.
Hata hivyo, mwaka
1932 aliendelea na
masomo kwa njia
ya posta ambapo
mwaka 1934 alitunukiwa
diploma ya fasihi.
Mwaka 1936 mpaka 1937 alitunukiwa cheti
cha English level.
Ni dhahiri
kuwa kama si
kubanwa na wakoloni
Shaaban Robert angekuwa
msomi mkubwa. Juhudi
zake za kutafuta
elimu ziliambata na
kunyimwa fursa ya
kwenda ng’ambo kusomea fasihi
ya Kingereza. Shaaban Robert
alifanya kazi mbalimbali enzi za uhai wake.
Ilipofika mwaka 1926,
alianza kazi katika
Idara ya Forodha
Tanga. Hapo alidumu
kwa muda wa
miaka takribani 18.
Mwaka 1944 – 1946 alihamishiwa idara ya wanyamapori huko
Mpwapwa. Mwaka 1946
alirudishwa Tanga na kuwa
afisa ardhi wa
jimbo la Tanga.
Aidha barua zake
zinaonyesha kuwa alifanya
kazi katika mikoa
ya Kilimanjaro, Arusha
na Pwani (Dar es
Salaam na Kisiju).
Kufanya kazi kwa
miaka mingi chini
ya utawala wa
kikoloni ni ithibati
kubwa ya umahiri
na uaminifu wake
katika utendaji wake.
Maisha yake
ya kazi yalivuka
mipaka ya utumishi
wa serikali ya
kikoloni kwa manufaa
yao hadi kwenye
shughuli za kukuza
na kukiendeleza Kiswahili
kwa manufaa ya
wazawa. Hakuchelea kuwa
mwanachama wa East
African Swahili Committee,
East Africa Literature
Bureau na Tanganyika
Language Board. Tumeelezwa
kuwa Shaaban Robert
alikuwa mwenyekiti wa
kamati ya Kiswahili
ya Afrika Mashariki
kutoka Novemba 1961
hadi alipofariki 1962
baada ya kifo
chake nafasi hiyo
ilichukuliwa na bwana
J.W.T Allen.
Mulokozi (2008)
anapoeleza maisha ya
ndoa ya Shaaban
Robert anasema, Shaaban
Robert alioa mke
wa kwanza, Amina
bint Kihere kati
ya mwaka 1930
na 1931. Alizaa
naye watoto kadhaa,
lakini wote walifariki
dunia isipokuwa wawili
Mwanjaa na Sulemani.
Bi. Amina naye alifariki takribani mwaka 1942. Baada
ya kifo cha
Amina, Shaaban Robert
alimuoa Bi Sharifa
binti Hussein mwaka
1945. Huyu alizaa
naye watoto wengi
lakini waliojaliwa kuishi
hadi utu uzima
ni Akili, Hussein,
Mwanamwema na Ikbal.
Bi Sharifa alifariki
mwaka 1955, Shaaban
Robert akamuoa Mwanambazi
binti Ali, ambaye
aliishi naye hadi
mauti ilipomkuta mwezi
Juni mwaka 1962.
Bi. Mwanambazi hakuzaa naye,
na alifariki mwaka
1964.
Anaendelea kueleza
kuwa Mwanamwema mama
yake na Shaaban
Robert alifariki dunia
mwaka 1967. Selemani
mwanae Shabaan Robert
alifariki miaka 1950
wakati akisoma shule.
Mwanamwema alifariki mwaka
1971, Mwanjaa bint
Shaaban Robert alifariki
dunia mwaka 1973,
Hussein alifariki mwaka
1992 na Akili
alifariki Januari mwaka
2007.
Shaaban Robert
aliandika kazi nyingi
za kifasihi hasa
ushairi na nathari.
Baadhi ya kazi
za ushairi alizoziandika
ni pamoja na Pambo
la Lugha, Koja
la Lugha, Mwafrika
Aimba, Almasi za
Afrika, Insha na
Mashairi, Kielelezo cha
Fasili, Ashiki Kitabu
Hiki, Masomo yenye
Adili, Mapenzi Bora,
Tenzi za Marudi
Mema na Omary
Khayyam, Utenzi wa
Vita vya Uhuru
na Almasi za
Afrika na Tafsiri
ya Kiingereza. Vitabu
vya kinathari ni
pamoja na Maisha Yangu
na Baada ya Miaka
Hamsini, Kusadikika, Utubora Mkulima,
Adili na Nduguze,
Kufikirika, Siku ya
Watenzi Wote, Kielelezo
cha Insha na
Wasifu wa Siti
binti Saadi.
Shaaban Robert
aliandika kazi nyingi
za kifasihi kutokana
na kwamba alitekwa
na dhamiri ya
kweli ya uandishi
katika maisha yake
yote ukirejelea kitabu
chake cha Maisha
Yangu na Baada
ya Miaka Hamsini
(2013: 65) anadhihirisha dhamira
yake ya uandishi
anasema:-
“Mauti huua
mwili wa Mwaandishi
ukawa vumbi tupu
kaburini. Lakini mchoro alioandika
wakati wa maisha
yake hudumisha uhai
wa jina lake duniani milele.
Kwangu mimi jambo hili
lilikuwa ni bora
kuliko fedha na dhahabu ya
ulimwengu.”
Ni wazi
dhamiri yake imetimia
kwa sababu jina
lake linaishi katika
fikra na mawazo
ya kizazi kimoja
hadi kingine. Hadi
sasa utafiti umeibua
kazi nyingine mpya
na kutimiza idadi
ya kazi zipatazo
24 ambazo zimetoa
na zinaendelea kutoa
mchango mkubwa katika
fasihi ya Kiswahili
ya hivi leo.
Hata kupelekea kupata
jina la baba
wa fasihi ya
Kiswahili.
1.1 Nadharia ya Uchambuzi
Nadharia ni
mwenga au msingi
ambao humsaidia mtu
katika kueleza mawazo
yake katika makala
haya tutatumia nadharia
ya mguso.
Ntarangwi (2004:19)
anaeleza kuwa nadharia
hii huitazama fasihi
katika uhusiano wake
na umma wake
ambapo msisitizo unatiliwa
mguso unaotolewa na
kazi ya fasihi
kwa hadhira yake.
Kila kazi ya
fasihi hulenga kwa
njia moja au
nyingine, mtu au watu
fulani (hadhira) hata kama hadhira
hiyo ni nafasi
ya mtunzi husika.
Kazi ya fasihi
hutoa mguso wa
aina fulani kwa
hadhira ili ifikirie
na kujiuliza maswali
au hata kutoa
funzo fulani. Akimunukuu Vasquez, A.S (1973:113) anasema:-
Kazi
ya sanaa huathiri
watu na inachangia
katika kuhimiza au
kupuuza dhana zao, maazimio yao,
hata maadili yao.
Ina msukumo wa
kijamii ambao huathiri
watu kwa nguvu
zake za kihisia
na kiitikadi. Ama
kwa hakika hakuna
anayebaki vilevile baada ya
kuguswa na kazi
halisi ya sanaa.
(Tafsiri
ya Ntarangwi)
Wanachokisisitiza hapa
ni kwamba kazi
yoyote ya fasihi
hutoa mguso fulani
kwa hadhira lengwa.
Lengo la
kutumia nadharia hii ni kuwa
kuna mguso kati
ya kazi ya
fasihi na hadhira
lengwa. Vilevile kuna
uwezakano mkubwa mwandishi
kuleta mguso katika
fasihi lengwa kwa
mfano Shaaban Robert
ametoa mchango mkubwa
katika fasihi ya
Kiswahili hivyo kuiendeleza
na kuipa sura
mpya fasihi ya
Kiswahili kutokana na
kazi mbalimbali za kifasihi
alizoziandika hadi kufikia
kuitwa baba wa
fasihi ya Kiswahili.
Hivyo nadharia hii itafaa katika
uchambuzi wa makala
haya.
1.2 Mchango wa Shaaban
Robert katika Ulimwengu wa Fasihi ya Kiswahili
1.2.1 Utangulizi
Katika kuangalia
mchango wa Shaaban Robert katika
fasihi ya Kiswahili
tutachunguza mambo kadha
wa kadha aliyoyafanya
mwandishi huyu hata
kuleta athari chanya
katika fasihi ya
Kiswahili na kufanya
kukumbukwa hadi leo
kama baba wa
fasihi ya Kiswahili.
1.2.2
Mchango wake katika Ulimwengu wa Fasihi
ya Kiswahili
Shaaban Robert
ameandika vitabu vingi
vya kifasihi vya
ushairi pamoja na
nathari. Katika upande
wa tungo za
ushairi inasemekana ndiye
mwandishi mwenye tungo
nyingi kuliko mwandishi
yeyote katika Afrika
Mashariki kwani ana
vitabu vya ushairi
alivyoviandika enzi za
uhai wake takribani
kumi na vinne
na utafiti bado
unaendelea kutafiti kuhusu
maandiko yake ambayo
hayajachapishwa. Katika upande
wa nathari ana
vitabu takribani kumi
ambavyo ameviandika.
Uandishi huo
umeleta tija kubwa
katika fasihi ya
Kiswahili ya leo
kwani baadhi ya vitabu vyake
vinatumika katika mitaala
ya elimu mfano
katika elimu ya
sekondari vitabu kama
vile Kufikirika, Kusadikika na Mapenzi
bora. Pia katika
vyuo vya ualimu
Daraja la tatu
A na vyuo vya Diploma
wanasoma vitabu vyake,
na hata katika
elimu ya vyuo
vikuu wanasoma vitabu
vyake mathalani Chuo
Kikuu cha Dar
es Salaam kuna
kozi maalumu inayohusiana
na uhakiki wa
maandishi ya Shaaban
Robert.
Hii inatokana
na kuwa maandiko
yake yana tija
kubwa kwa wanajamii
kwani yalijaa mafunzo
kiasi kwamba kwa
mtu yeyote makini
anaposoma kazi zake
ni lazima apate
athari chanya na
kuweza kumsaidia katika
maisha yake.
Mbali ya
vitabu vyake kutumika
katika kutolea maarifa
vitabu hivyo vimesambaa
sehemu mbalimbali katika
nchi za Afrika
Mashariki na hivyo kuifanya fasihi
ya Kiswahili kusambaa
maeneo mbalimbali ya
ulimwengu na hata
kushika hatamu.
Shaaban
Robert alikuwa mzalendo wa lugha ya Kiswahili.
Kama inavyojulikana alifanya
kazi katika kipindi
cha ukoloni na
lugha iliyokuwa inasisitizwa
ni lugha ya
Kiingereza. Lakini aliweza
kuandika kazi zake
za kifasihi kwa
Kiswahili na hivyo kukuza
fasihi ya Kiswahili.
Tukimrejelea Ruhumbika (1983:259) katika Utangulizi wake anasema:
Inaeleweka kuwa
fasihi ni sehemu
muhimu sana ya
utamaduni wa binadamu. Halafu ni
mojawapo ya vyombo
vikuu vya ukuzaji
wa lugha. Lugha bila fasihi inayokuwa nayo
haiwezi kukua. Hali
hii ilikuwa inaeleweka
wakati wa ukoloni kwani mkoloni
alielewa sana kwamba
lugha bila fasihi
ni lugha ambayo
haifiki popote,na kwamba
ukitaka kuua utamaduni
fulani unyang’anye utamaduni
huo sanaa zake.
Ni wazi
kuwa Shaaban Robert
alilitambua hilo na
kuamua kulipigania kwa
kuandika kazi zake
katika lugha ya
Kiswahili ili kuweza
kukuza fasihi ya
Kiswahili na hili
linajidhihirisha katika maandiko
yake mengi ambapo
anasisitiza umuhimu wa
kutumia lugha ya
Kiswahili mathalani katika
andiko lake la Mwafrika
Aimba katika shairi
la “ lugha yetu” uk. 33
– 34 anaonesha mapenzi ya lugha
ya Kiswahili anasema:-
Lafidhi ina
fahari, kutetea ndio
utu, Kukosa lugha
hatari, uliza kila
mtu, Mwelewa wa
kufikiri, atajibu ni
kuntu, Hima wakutane
watu, au tutahasiri.
Shaaban Robert
alikuwa tayari kukitetea
Kiswahili mahali popote
na kwa gharama yoyote hii
ilitokana na uzalendo
aliokuwa nao mwandishi
huyu. Ni wazi
kuwa Shaaban Robert
hakuwa mahiri wa
lugha ya Kiswahili
tu bali hata
lugha ya Kiingereza
na Kiarabu. lakini
msisitizo aliuweka katika
lugha ya Kiswahili
na hii inajidhihirisha wazi
katika andiko hilo
anaposema:-
Lugha ngeni
na makini, zina
manufaa kwetu, Tujifunze kwa
dhamiri, tuseme kama
upatu, Walakini tufikiri,
ubora wa lugha
yetu, Hima
wakutane watu, au
tutahasiri.
Mwandishi huyu
alitambua umuhimu wa
kujifunza lugha nyingine
lakini msisitizo ukiwa
katika lugha ya
Kiswahili, tofauti na
ilivyo kwa watu
wengi wanaoweka msisitizo
katika lugha za
kigeni kuliko lugha
zao. Kwani mwandishi
huyu angeweza kuandika
katika lugha ya
Kiingereza lakini kutokana
na uzalendo wake
katika Kiswahili aliamua
kuandika kwa lugha
ya Kiswahili ili
kukuza fasihi ya
Kiswahili na laiti
angetumia lugha ya
Kiingereza fasihi ya
Kiswahili isingeweza kupiga
hatua kama ilivyo
leo hii.
Shaaban Robert
ni miongoni mwa
waasisi wa mwanzo
wa fasihi ya
Kiswahili aliyeeneza fani
ya riwaya katika
Kiswahili ingawa alitanguliwa
na J. Mbotela na A.
Kiterezaa. Licha ya
kutanguliwa na waasisi
hao lakini yeye
aliandika kazi nyingi
za kifasihi kuliko
wao kwani mpaka
sasa yasemekana kuna
kazi takribani 24
na bado kuna
madai yanayosema kuwa
zipo kazi nyingi
za Shaaban Robert
ambazo hazijachapishwa na
kupelekea kuwapo kwa
tafiti mbalimbali zinazofanywa
ili kubaini kazi
hizo. Hivyo ni
wazi kuwa aliweka
msingi katika fasihi
ya Kiswahili hasa
fasihi andishi na
kupelekea fasihi ya
Kiswahili kukua na
kuenea sehemu mbalimbali
kupitia maandiko yake.
Hivyo ni
wazi fasihi ya
Kiswahili ya hivi
leo imetokana na
jitihada za gwiji
huyo pamoja na
wengine kuhakikisha kuwa
fasihi ya Kiswahili
haipotei.
Shaaban Robert
ameweka kiungo kati
ya fasihi simulizi
na fasihi andishi,
ambapo alikutanisha fasihi
simulizi na fasihi
andishi kwa kutumia
vipengele mbalimbali vya
fasihi simulizi katika
fasihi andishi mathalani
katika kazi zake
za Adili na Ndunguze,
Kufikirika, Kusadikika na Siku
ya Watenzi Wote. Katika kazi
hizi mwandishi ametumia
nduni za kifasihi
simulizi mfano wahusika
bapa wasiobadilika kutoka
mwanzo wa hadithi
hadi mwisho wa
hadithi, mianzo na
miisho ya kifomula,
matumizi makubwa ya
wahusika wasiokuwa binadamu
na matumizi makubwa
ya takiriri. Hali
hii inasawiriwa sasa
katika fasihi ya
Kiswahili ya hivi
leo kwa kutumia
dhana ya fasihi
ya Kiswahili ya
Majaribio.
Senkoro (2011:62-81)
anapoelezea juu ya
fasihi ya Kiswahili
ya majaribio anasema
hakuna upya wowote
kwani vipengele vinavyotumika
katika fasihi ya
Kiswahili ya hivi
leo vilishajaribiwa na
kutumiwa na waandishi
kama Shaaban Robert
katika kazi zake
zake za Kusadikika, Kufikirika
na
Adili na
Ndunguze. Kiasi kwamba
inakuwa vigumu kuona
upya wa majaribio
ya Kezilahabi, Mohamed
na waandishi wengine
wa kisasa wanaotumia
mtindo wa uhalisiamazingaombwe:, mtindo
ambao ni kama
pombe ya zamani
katika kibuyu kipya.
Hivyo ni
wazi kuwa Shaaban
Robert ndiye aliyeanzisha
mtindo huo na
hata kuleta athari
kubwa kwa waandishi
wengine ambao nao
wameanza kuandika kama
yeye. Kuzuka kwa fasihi
ya Kiswahili ya
majaribio katika miaka
ya (1980) ambapo waandishi
wa hivi leo
wanatumia nduni za
kifasihi simulizi katika
fasihi andishi mfano
kazi kama Lina Ubani (P.
Muhando), Jogoo Kijijini na
Ngao ya Jadi (E.
Hussein) na pia riwaya
ya Rosa Mistika hii
inatokana na mchango
mkubwa wa mwandishi
huyu katika fasihi
ya Kiswahili.
Shaaban Robert
amehusika katika kuingiza
fani ya tafsiri
katika lugha ya
Kiswahili na kuonesha
kuwa alikuwa Mtaalamu
mzuri wa kutafsiri
mfano katika andiko
lake la Almasi za
Afrika Katika kitabu hiki
mashairi yametafsiriwa katika lugha ya Kiingereza. Kwa mujibu wa Shaaban Robert
mwenyewe anasema katika utangulizi kuwa kusudi la tafsiri za Kiingereza katika kitabu
hiki ni kuonyesha jinsi Kiswahili kiwezavyo kuchukuana vyema na lugha
nyingine na pia kusaidia
baadhi ya wasomaji kuelewa kuwa
Kiswahili si lugha maskini.
Pia alitafsiri
kazi ya Omary Khayyam
kutoka katika lugha
ya Kiingereza iliyokuwa imetafsiriwa
na Fitzegerald ya
Rubaiyat. Na hii
pia ilitokana na
kuwa kazi ngeni
inaweza kuwa na
tija katika fasihi
ya taifa fulani
hivyo kupelekea kazi
hiyo kuitafsiri kama
mwandishi mwenyewe anavyoeleza
kuwa kazi hiyo ilikuwa na
tija katika jamii
zetu kwani yaliyoelezwa
yaliendana sambamba na
jamii zetu na
hii ilichochea suala
la tafsiri katika
fasihi ya Kiswahili
kwani watu mbalimbali
walianza kutafsiri kazi
za kifasihi kutoka
lugha za kigeni
kuja katika lugha
ya Kiswahili mfano
Mwalimu J. K. Nyerere alitafsiri
vitabu viwili vya
mwandishi mashuhuri wa
tamthilia wa Uingereza,
William Shakespeare. Tafsiri
hizo ni Juliasi Kaizari
na Mabepari wa Venisi.
Naye Paul Sozigwa
alifasiri kitabu cha Song
of Lawino na
kukiita Wimbo wa Lawino.
Tukiwarejelea Mwansoko
na wenzake (2006) Wanaeleza
kuwa baada ya
uhuru wananchi wengi
waliokuwa na ujuzi
wa lugha za
kigeni walifasiri maandiko
mbalimbali muhimu ya
lugha hizo kwa
Kiswahili ili kuwasambazia
wazalendo wenzao maarifa
na taaluma zilizokuwemo
katika maandiko hayo.
Matokeo yake
ni kwamba hivi
leo Kiswahili kina
hazina ya taaluma
na fasihi ikiwemo.
Hivyo, ni wazi
Shaaban Robert alitoa
mchango mkubwa katika
kuingiza fani ya
tafsiri katika fasihi
ya Kiswahili na
kupelekea ongezeko kubwa
na ufanyaji wa
tafsiri katika fasihi
ya Kiswahili ya
hivi leo mbali
na changamoto zilizopo
katika kufasiri kazi
za kifasihi.
Shaaban Robert
alikuwa na uwezo
mkubwa katika kutumia
lugha. Aliandika kazi
zake kwa kutumia
mbinu nyingi za
kifani hata kufikia
mahali baadhi ya
watu kudai kuwa
kazi zake ni
za kufikirisha mno
na hazina maana
yoyote katika jamii
lakini ni wazi
kuwa kazi zake
zina tija katika
jamii zetu. Madai
hayo yalitokana na
ufundi mkubwa aliokuwa
nao katika utumiaji
wa lugha mfano
namna ya uumbaji wa
wahusika, madhari, matumizi
ya tamathali za
semi pamoja na
mbinu ya ufutuhi.
Hivyo kupelekea
kuibuka kwa watunzi
wengine katika fasihi
ya Kiswahili ya hivi leo
wanaotumia mbinu nyingi
za kifani na
kufanya kazi zao
kuwa vigumu kuzielewa
mathalani E. Kezilahabi
na S. Mohamed kazi
zao huwa na
mbinu nyingi za
kifani. Hii hufanya
fasihi ya Kiswahili
kuendelea kukua na
kuwafikirisha wasomaji ili
kuweza kupata funzo
kutokana na kazi
hizo.
Shaaban Robert
aliweza kueleza matukio
ya kweli kwa
kutumia ubunifu katika
baadhi ya kazi
zake, mathalani riwaya
ya Wasifu wa Siti
binti Saad, Utenzi wa
Vita vya Uhuru
na katika Maisha yangu
na Baada ya
Miaka Hamsini. Licha
ya kwamba baadhi
ya watu walikuwa
wakimpinga kuwa huo
haukuwa ubunifu. Lakini ni
wazi kuwa ubunifu
ni dhana yenye
maana mbili kwanza
unaweza kuumba kazi
ya fasihi kutokana
na mambo ya
kibunifu au mambo
ambayo hajapata kutokea
duniani na pili
unaweza kutengeneza kazi
ya fasihi kwa
kutumia matukio ya
kweli lakini yanakuwa
na usanii.
Tukimrejelea
Dkt. Samwel Method, “Maandiko ya
Shaaban Robert na
Uhalisia na Ubunifu”
mhadhara uliotolewa Chuo
Kikuu cha Dar-es-Salaam, 16 Januari, 2014,naeleza kuwa
Shaaban Robert anapoeleza
matukio ya ukweli
anatumia sana mbinu
za kifani. Mbali
na kazi ya
kifasihi kuwa ya
kibunifu ni wazi
kuwa mwandishi hawezi
kwenda nje ya
jamii yake na
huaminika kwamba watunzi
wengi wa kifasihi
huathiriwa sana na
maisha yao. Anahitimisha
kwa kueleza kuwa
Shaaban Robert alikuwa
ni mwandishi mahiri
na mbunifu.
Hali hii
ya kuandika mambo
ya kweli kwa
kutumia ubunifu imeanza
kutumiwa na waandishi
wa fasihi ya
Kiswahili ya hivi
leo mathalani kazi
nyingi za Mulokozi
kama vile Moto wa
mianzi, Ngome ya
Mianzi, Ngoma ya
Mianzi, Mukwava wa
Uhehe na Utenzi wa
Nyakiiru Kibi. Ni
kazi zinazohusu matukio ya
kweli yaliyowahi kutokea
lakini mwandishi huyu
ametumia ubunifu.
Lengo hasa
ni kuonesha kuwa
fasihi ina uwezo
mkubwa wa kubeba
historia iwe ya
mtunzi binafsi au
jamii kwa ujumla. Hivyo
ni wazi kupitia
Shaaban Robert anapanua
mwanya na kuibuka
watunzi wengine wapya
katika kueleza mambo
ya kweli lakini
kwa kutumia ubunifu
na hii hupelekea
fasihi ya Kiswahili
kuzidi kukua.
1.3 Hitimisho
Ni wazi
kuwa Shaaban Robert
alikuwa mwandishi mahiri
na mbunifu wa
kazi za kifasihi
kwa wakati ule
lakini kazi hizo
zimeleta mguso katika
fasihi ya Kiswahili
ya hivi leo
kwani kazi zake
zinaendelea kutumika katika
taasisi mbalimbali za
elimu na bado
zina mafunzo katika
jamii zetu za
sasa mbali na
hiyo hata kupelekea
waandishi wengi wa
sasa kufuata nyayo
zake kwa kujaribu
kuandika kama yeye.
Hivyo kutoa mwanya
kwa fasihi ya
Kiswahili kuendelea kukua
kwa kasi.
Kutokana na
umuhimu wa gwiji
huyu taasisi za
elimu ya juu
zinafanya tafiti mbalimbali
kuhusiana na Shaaban
Robert ili kuweza
kubaini kazi zake
nyingine ambazo bado
hazijachapishwa mathalani utafiti
uliofanywa na Mulokozi
na Shani Kitogo
juu ya maisha
ya Shaaban Robert
na kazi zake
na mapato ya
tafiti hizo ni
pamoja na Barua za
Shaaban Robert kilichoandikwa na
Mulokozi (2002) na Mithali na
mifano ya Kiswahili
(utafiti uliofanywa na
Shani Kitogo na
Mulokozi).
MAREJEO
Chuachua, R. (2011). Itikadi katika Riwaya
za Shaaban Robert.
Dar es Salaam:
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.
Method, S.
“Maandiko ya Shaaban
Robert na Uhalisia
na Ubunifu” mhadhara
uliotolewa Chuo
Kikuu cha Dar-es-Salaam, 16 Januari, 2014.
Mulokozi, M . M (2008).
Utang. Siku ya Watenzi
Wote. Dar es
Salaam: TUKI.
Mwansoko na
wenzake (2006). Kitangulizi cha
Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar es
Salaam: TUKI
Ntarangwi, M. (2004).
Uhakiki wa
Kazi za Fasihi.
Augustana College: Rock
Island.
Robert, S. (1946).
Mwafrika Aimba.
Nairobi: Nelson.
Robert, S. (2013).
Maisha yangu
na Baada ya
Miaka Hamsini. Dar
es Salaam: Mkuki na Nyoka
Publishers.
Ruhumbika,
G. ( 1983). “Tafsiri za
Fasihi za Kigeni
katika Ukuzaji wa
Fasihi ya Kiswahili”
katika Fasihi, Juz. III Makala za Semina
ya Kimataifa ya
Waandishi wa Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI. Uk 259- 272.
Senkoro,
F.E.M.K. (2011). Fasihi. Dar es
Salaam: KAUTTU Ltd.