Kurasa Muhimu

Thursday, January 10, 2013

RIPOTI YA KONGAMANO LA 6 CHAWAKAMA KANDA YA TANZANIA LILILOFANYIKA MUCE-IRNGA



Shukrani
Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa wale wote walioshirikiana nasi hadi kufanikisha kuhudhuria kongamano hili. Kwa kweli ilikuwa ni changamoto kubwa kufanikisha kuhudhuria katika kongamano kutokana na uhaba wa pesa tulio nao. Pamoja na changamoto hizo lakini uongizi wa chawakama ulithubutu kumpeleka kiongozi mmoja ili kuwakilisha tawi letu, tunawashukuru sana.
Vilevile tunawashukuru sana wanachama waliojinyima na kuamua kutumia pesa kwenda MUCE ili kuwakilisha tawi letu, mmetujengea heshima kubwa, tunawashukuru sana.
Mwisho kabisa tunapenda kumshukuru Katibu msaidizi kwa moyo wake wa kujitolea, kutokana na ukata unaoukabili CHAMA, aliamua kutumia pesa zake ili kufanikisha kuhudhuria katika kongamano.
Utangulizi
CHAWAKAMA-UDSM imekuwa mstari wa mbele katika kuhakisha malengo ya chama yanasonga mbele. Uwakilishi wetu katika makongamano umekuwa ni mzuri sana. Tangu kongamano la kwanza (1) la kanda hadi hili la sita (6) tumekuwa na uwakilishi katika kila kongamano, japokuwa idadi ya wawakilishi inakuwa ndogo lakini angalau tunakuwa na uwakilishi.
Kwa kuzingatia mlolongo huu wa kuandaa makongamano, kongamano la 6 limefanyika katika Chuo Kikuu kishiriki Cha Mkwawa (MUCE). Kama ilivyokawaida yetu sisi CHAWAKAMA-UDSM katika kutimiza majukumu muhimu ya chama, tulituma uwakilishi katika kongamano hili. Jumla ya washiriki kutoka tawi letu waliohudhuria ni wanne (4). Kiongozi mmoja na wanachama wa kawaida watatu. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanachama zaidi ya 100 tulionao lakini sababu pekee ya idadi hii ni kutokana na uhaba wa pesa tulionao.
Kwa hiyo ripoti hii ina lenga kuelezea kile kilichojiri katika kongamano la 6 lililofanyika MUCE-Iringa.
KONGAMANO LENYEWE
Kongamano la 6 la kitaifa la CHAWAKAMA mwaka 2013 lilifanyika katika chuo kikuu kishiriki cha Mkwawa (MUCE) – Iringa. MUCE ndio walio kuwa wenyeji wa kongamano la 6 mwaka 2013.
Washiriki kutoka vyuo mbalimbali vya Tanzania walihudhuria ikiwa ni pamoja na washiriki kutoka shule ya Sekondari Mlamke. Washiriki wa kongamano walianza kuwasili tarehe 20 Feburuari kutoka katika vyuo mbalimbali kutoka maeneo tofautitofauti ya Tanzania. Miongoni mwa vyuo hivyo Chuo kikuu cha Dar es Salaam hakikuwa nyuma na kiliwakilishwa na wanachama wanne. Baada ya kuwasili tulikaribishwa kwa bashasha na wenyeji wetu na siku hiyo ilikuwa ni siku ya maadalizi kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa kongamano.
Tarehe 21 Feburuari ndio ilikuwa siku rasmi ya ufunguzi wa kongamano. Kabla ya kuingia ukumbini asubuhi ya siku hiyo kwa ajili ya ufunguzi rasmi tulifanya maandamano kwa kuimba nyimbo za kukitukuza Chama chetu. Baada ya kuingia ukumbini tuliketi chini na kumsikiliza Manju ili kujua kile kilichokuwa kinafuata kwa mujibu wa ratiba ya siku hiyo.
Ilipotimia saa 3 asubuhi kongamano lilifunguliwa rasmi. Mgeni rasmi wa kongamano alikuwa ni Makamu Meya (Deputy Mayor) wa Manispaa ya Iringa Ndugu Gervance Ndaki ambaye alikuja kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Iringa.
Baada ya ufunguzi huo ilifuata risala iliyosomwa na Mwenyekita wa Kanda ya Tanzania kwa mgeni rasmi. Risala hiyo ilihusu maendeleo ya chama kwa ujumla ambayo ni mazuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo Kiswahili hakikuwa na hadhi ya juu ukilinganisha na sasa ambapo tunaona Kiswahili kimenea na kukua kwa kasi sana. Pamoja na mafanikio hayo pia risala ilionesha jinsi chama kinavyokabiliwa na changamoto. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa fedha kwa ajili ya kuendeshea chama, kwa mfano kushindwa kuandaa makongamano kwa fedha za chama na badala yake tunategemea malipo yanayofanywa na wanachama, hii inamaana kwamba bila wanachama kuchangia hatuwezi kuandaa kongamano. Pia kutokana na uhaba wa fedha chama kimeshindwa kusajiliwa mpaka hivi sasa kitu ambacho ni tatizo kubwa kwa kutotambulika kwa chama chetu kisheria.