HISTORIA KWA UFUPI YA
UKUTA (USANIFU WA KISWAHILI NA USHAIRI TANZANIA) MALENGO YAKE NA UMUHIMU
WAKE
Mada iliyowasilishwa na
Ndugu Abdallah Ahmad Seif (Ngome Imara) katika kongamano la CHAWAKAMA
lililofanyika Tarehe 30/8/2012 – 01/09/2012
Ngozi, Burundi
Chama au chombo cha UKUTA (Usanifu wa Kiswahili na Ushairi
Tanzania), kiliasisiwa Tarehe 29/3/1959 Mjini Dar es salaam na wapenzi wa Lugha
ya Kiswahili pamoja na Ushairi, Mwenyekiti wa chama Taifa akiwa marehemu
Mahamoud Hamdouny (Jitukali), aliyekuwa mshairi maarufu katika ukanda huu wa
Afrika ya mashariki na pia mjuzi mkubwa aliyebobea wa lugha ya Kiswahili ambaye
maskani yake yalikuwa mjini Dodoma.
Watu wengine maarufu ambao walikuwa ni waasisi wa chombo hichi
UKUTA, ni akina Mzee Mathias Mnyampala, Shaaban Robert, Sheikh Kaluta Amri
Abeid, Mzee Akilimali (Snow white), Mzee Mwinyikhatibu Mohammed, Mzee Said
Shomari Kaniki na wengineo wengi.
Mara baada ya Tanzania (Tanganyika) kupata Uhuru, UKUTA ulipata
nguvu zaidi baada ya kuongezeka wadau wengi wapenzi wa Lugha ya Kiswahili,
akiwemo Rais wa kwanza wa Tanzania marehemu Mwl. Julius Kambarage Nyerere,
ambae alikuwa mdau mkubwa wa Lugha ya Kiswahili na pia Mshairi alieumudu vema
Ushairi.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati huo ndiye aliyekuwa mlezi wa
chama cha UKUTA, na kwa nafasi yake alitoa chumba kimoja katika jengo la Anatouglo
Dar es salaam ili kitumike kama ofisi kuu ya UKUTA. Ofisi hiyo ipo mpaka leo na
inaendelea kutumika kwa kazi mbalimbali za kiofisi za UKUTA.
UKUTA ilifungua matawi Mikoani, na hivyo kuwa chombo kilichokuwa
karibu na wananchi, na hivyo hamasa ya watu kukienzi Kiswahili ikawa iko juu
kutokana na mipango madhubuti iliyokuwepo wakati huo.
MALENGO YA UKUTA
Malengo ya UKUTA ni kama yalivyoainishwa katika katiba
yake ambayo ni pamoja na:-
i)
Kulinda, kuhifadhi na
kustawisha Lugha ya Kiswahili, Ushairi na Utamaduni wake.
ii)
Kufanya kazi zitakazostawisha
Ushairi kuwa sehemu ya mitaalaa ya Kiswahili nchini na nje ya nchi na kukuza
Kiswahili kwa kuzingatia Lugha za kibantu.
iii)
Kuhamasisha na kuamsha ari na
kuwasaidia watu wanaotaka kuwa mafundi wa lugha ya Kiswahili katika taasisi za
elimu na jamii kwa ujumla.
iv)
Kuhamasisha na kuamsha ari za
wale wanaotaka kutunga vitabu vya fani mbalimbali za elimu kwa lugha ya
Kiswahili na vya Ushairi na kutafuta njia za kuchapisha kazi zao.
v)
Kutunza, kulinda na kutangaza
kazi za Kiswahili zilizotungwa na watunzi waliokwisha kutangulia mbele ya haki.
vi)
Kusisimamia matumizi sahihi na
sanifu ya Lugha ya Kiswahili na kukosoa na kuelekeza pale Lugha ya Kiswahili
inapokosewa ili matumizi sahihi ya Kiswahili yabaki katika unyoofu wake.
vii)
Kufasiri matangazo, maandishi,
vitabu, filamu, kazi za sanaa kutoka Lugha za kigeni, Asili kwenda Lugha ya
Kiswahili.
viii)
Kutoa huduma ya ufasiri na
ukalimani katika mikutano ya Kitaifa na kimataifa.
ix)
Kushirikiana na taasisi
nyingine za ndani na nje ya nchi yetu katika kukiendeleza Kiswahili.
UMUHIMU WA UKUTA
UKUTA ni chombo muhimu kutokana na malengo kiliyonayo katika
uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili na sanaa ya Ushairi.
Hivyo ni muhimu kwa wadau wa Kiswahili kujiunga na chombo hichi,
kuanzia wanafunzi wanavyuo, na watu wengine wa kada mbalimbali.
Kwani mnapokuwa katika chombo kilichosajiliwa na kutambulika na
chenye historia adhimu katika Tasnia ya Kiswahili, inakuwa ni rahisi
kuunganisha nguvu zenu kupitia chombo hicho na kuweza kuyafikia malengo yenu.
Kwa kuzingatia changamoto nyingi zinazowakwaza wadau wa Lugha ya
Kiswahili kutokana na kukosa msukumo kutoka Serikalini, ni vyema wadau wa
Kiswahili wakiunganisha nguvu kupitia katika chombo, wanaweza kuyafikia malengo
yao, tofauti na mtu ukiwa mmoja mmoja, siyo rahisi kusikika na kutekelezewa
jambo lako hata kama hicho unachokidai kina mantiki ndani yake.
CHANGAMOTO ZILIZOIKUTA
UKUTA
Changamoto zilizoikuta UKUTA na kusababisha kulegalega, kwa sehemu
kubwa zilichangiwa na viongozi wenye mamlaka katika utawala wa nchi kutokipa
uzito Kiswahili katika umuhimu wake, na hivyo kusababisha hata zile taasisi
zilizokuwa zinasimamia malengo ya kukiendeleza Kiswahili zipoteze mwelekeo.
Taasisi hizo kama UKUTA zilizokuwa na umuhimu mkubwa katika
maendeleo ya Lugha ya Kiswahili, zilishindwa kujiendeleza kwa ufanisi kwa
sababu ya kukosa nyenzo muhimu, ikiwa ni pamoja na fedha.
Serikali iliyopaswa kuzisaidia taasisi hizi kwa maendeleo ya lugha
adhimu ya Kiswahili, haikuchukua wajibu wake huo muimu, na hivyo kuziacha
taasisi hizi katika hali ngumu, zikikabiliwa na ukata, na hivyo kukwamisha
malengo ambayo taasisi hizi zilikuwa zimejiwekea.
Lakini kwa kuwa UKUTA ni taasisi yenye malengo mazuri kwa mustakabali
endelevu wa lugha ya Kiswahili, WANAUKUTA waliendelea na juhudi zao. Pamoja na
kukosa uungwaji mkono kutoka katika mamlaka za utawala, juhudi za kukiendeleza
Kiswahili pamoja na sanaa ya utunzi wa Mashairi ziliendelezwa hadi kufanikisha
kuchapisha vitabu kadhaa vya mashairi na hata vitabu vingine vya Kiswahili
vyenye maudhui mbalimbali yenye kuifaidisha jamii.
Mfano wa vitabu hivyo ni, DIWANI YA MLOKA ambayo kwa miaka mingi
kuanzia 1998 hadi mwaka 2008 ilitumika kufundishia shuleni. Pia kuna vitabu
kama ADHA YA UKIMWI, ELIMU YA JAMII NA CHEMSHA BONGO na vingine vilivyotungwa
kwa Lugha ya Kiingereza vyenye maarifa ya kutosha, vilivotungwa na MWANAUKUTA
ambaye ni Katibu wa UKUTA tawi la Dodoma,
ndugu Charles Mloka.
Vingine ni BAHARI YA HEKIMA YA USHAIRI kilichotungwa na Mshairi
maarufu nguli, Amiri Sudi Andanenga.
Kwa kuwa juhudi za kuliendeleza jambo lolote, huwa zipo kwa wahusika
wenyewe wenye jambo lao hilo. Wadau wa Kiswahili Dodoma tuliamua mwaka 2000, kukutana
na kulihuisha tena wa tawi la UKUTA kwa malengo ya kuendeleza Lugha yetu ya
Kiswahili na sanaa ya utunzi wa Mashairi baada ya tawi hili lililoanzishwa
mwaka 1960 kusuasua hasa mwishoni mwa mwaka 1990.
Hivyo Januari mosi mwaka 2000, tawi la UKUTA Dodoma llilifanya
uchaguzi na kupata viongozi wapya kama ifuatavyo:-
Mwenyekiti - Mariam Ponda
Makamu/M/Kiti - Ramadhani Nyembe
Katibu - Charles Mloka
Katibu Mwenezi - Abdallah Hancha
Mwenezi Msaidizi - Abdallah Seif
Mweka Hazina - Saleh Seif
Mohammed Kajembe - Mjumbe
Halidi Jumanne - Mjumbe
Mohamed Kiwipa - Mjumbe
Ayoub Seif - Mjumbe
Zainabu Issa - Mjumbe
Said Yasini - Mjumbe
Hamisi Biliyetega - Mjumbe
Justina Mwaja - Mjumbe
Mussa Kazimiri - Mjumbe
Juma Kidogo - Mjumbe
Said Kaniki - Mlezi
Kwa sasa angalau, kuna mwangaza unaojitokeza wa Lugha hii ya
Kiswahili na hata Sanaa ya Ushairi kupata msukumo kutoka kwa viongozi wenye
mamlaka ya utawala. Kwani kongamano la UKUTA lililofanyika Mjini BUKOBA, Mkoani
KAGERA, Tarehe 31 Machi hadi Tarehe 01 Aprili mwaka 2012, mkuu wa Mkoa huo
Mheshimiwa FABIAN MASSAWE alibeba jukumu la kuufadhili mkutano huo kwa juhudi
zake, na hivyo kuonesha angalau sasa viongozi wameanza kutambua umuhimu wa
uwepo wa taasisi za uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili na kuelewa kwamba
zinahitaji kuwezeshwa na kuungwa mkono ili kufikia lengo la Kiswahili
kufahamika vyema kwa wadau kitaifa na kimataifa ili kiwe hazina kwa maendeleo
endelevu.
UKUTA Dodoma imejipanga kutumia fursa zitazojitokeza za uungwaji
mkono kwa umakini na ufanisi. Tayari tuna mipango ya kutoa vitabu vya mashairi
na vitabu vingine vya Kiswahili vyenye maarifa na maelimisho kwa kushirikiana
na vyuo vikuu vya Dodoma (UDOM) na St. John, na tayari maandalizi ya kazi hizo
yameshaanza kufanywa.
Hivyo tunawakaribisha wote walio tayari katika kuliendeleza jahazi
letu la Kiswahili, kuungana nasi ili kufanikisha malengo yetu ya kukifanya
Kiswahili kuwa kweli ni hazina ya Afrika
kwa maendeleo endelevu.
SANAA YA USHAIRI
Sanaa ya Ushairi ni katika tanzu za fasihi za Lugha ya Kiswahili.
Ushairi ni Sanaa yenye historia ndefu na inaenda sanjari na historia ya Lugha
ya Kiswahili.
Ushairi umeanza chungu ya miaka, kwa ushahidi wa tungo za mashairi
za Bwana Muyaka bin Haji.
Kwamba Ushairi umeanza miaka mingi kabla ya wageni kuja katika
janibu yetu ya Afrika Mashariki. Hivyo basi Ushairi umeanza kuwepo kabla wageni
kutuijia kwenye pande zetu hizi na hivyo kuwa ushahidi tosha, kuwa ushairi asili
yake inaenda bega kwa bega na Lugha ya Kiswahili ambayo asili yake ni Kibantu. Hivyo
Sanaa ya ushairi tunapaswa kujivunia nayo kwani inatokana na sisi wenyewe. Ushairi
kwa miaka mingi umetumika katika kuielimisha jamii kwa maswala mbalimbali pia
kuiburudisha.
Katika Tanzania, washairi waliandika mashairi mbalimbali katika
kuhamasisha kudai uhuru wa Tanganyika na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika
harakati hizo. Hata baada ya Uhuru mashairi yalitumika katika kuwajenga watu
kuwa na uzalendo na nchi yao, na kuhamasisha watu kufanya kazi kwa bidii ili
taifa liweze kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.
Itoshe kusema, ushairi una faida kubwa katika jamii, kwani unaonya,
unaelimisha, unahamasisha mambo mazuri na pia kuburudisha. Hivyo ni muhimu watu
kujifunza Ushairi ili waweze kutunga mashairi na pia kuyasoma na kusikiliza,
kutokana na faida lukuki zilizosheheni katika sanaa hii ambayo huwa imepangwa katika
mpango unaovutia na kusisimua.
Ni vizuri sanaa hii ikarithishwa na kuendelezwa vizazi hadi vizazi
kwa kuwafundisha watu waijue na waipende kutokana na umuhimu na uadhimu
ilionao, ukizingatia ina mchango mkubwa katika uendelezaji wa Lugha ya Kiswahili.
Shairi hupangwa kwa urari wa
mizani na vina, huku maudhui yaliyotawala katika shairi yakiwa na mvuto na
msisimko mkubwa kutokana na mpangilio wa maneno yenye kufanana katika miishilio
yake. Ama hakika Sanaa hii ya Ushairi tunapaswa KUIDUMISHA.
Nimalizie kwa kusoma shairi hili nililolitunga ili kumpongeza na
kumuusia mshairi mwezetu ndg Mohamed Mkagile Mandai baada ya kufunga ndoa “MAISHA
YA NDOA YA MKAGILE” lililotoka katika gazeti la Uhuru Februari mwaka 1993 kama
mfano wa shairi zuri la kuvutia na lenye kudhihirisha uzuri na uadhimu wa Sanaa
ya Ushairi.
MAISHA YA NDOA YA MKAGILE
1.
Mkagile wa mandai, umeshaoa kijana,
Usia
ninatumai, huu nitaounena,
Najua
huukatai, nawaombea rabana,
Maisha
yawe mwanana, Mkagile wa Mandai.
2.
Ndoa natoa madai, ni safari ndefu sana,
Epukeni
ulaghai, dunia ulojazana,
Mpende wako
nisai, nae akupende bwana,
Hili
jambo la maana, Mkagile wa Mandai.
3.
Tamaa ni haifai, hiyo ni kuepukana,
Ridhini
Siwahadai, kitakacho patikana,
Mwenda pole
hajikwai, faraja huja kufana,
Tamaa
heri haina, Mkagile wa Mandai.
4.
Dhana kamwe haizai, jambo lenye muamana,
Muwe hilo
hamtwai, la mambo kudhaniana,
Penye dhana
hapang’ai, ushwari huwa hamna,
Mzingatie
kwa kina, Mkagile wa Mandai.
5.
Dhana kama hamwambai, nayo mkiambatana,
Welewano
haukai, kutadumu kuzozana,
Itazuka
jitimai, msisikizane tena,
Hatima
mtaachana, Mkagile wa Mandai.
6.
Maisha nawapa rai, muishi kwa kupatana,
Kama maji na
karai, kama nywele na kitana,
Ni kama suti
na tai, daima mkirandana,
Mambo
mkiridhiana, Mkagile wa Mandai.
7.
Kamwe msijikinai, mdumu kuelewana,
Furaha
haisinyai, mkiwa mmeshibana,
Faraka
haiwavai, kama mkishikamana,
Katika
zote namna, Mkagile wa Mandai.
8.
Nasi panapo uhai, tutakuja kuwaona,
Mje tukirimu
chai, na vitu vya kutafuna,
Mikate jamu
mayai, na vingi vyenye kunona,
Tukija
kwenu bayana, Mkagile wa Mandai.
9.
Atowapa vurumai, Mungu ampe laana,
Afe kwa
kizaizai, na maitiye kuchina,
Kisha iliwe na
tai, kuzikwa iwe hakuna,
Ataeleta
fitina, Mkagile wa Mandai.
10. Beti kumi baibai, kwa
nguvuze Rahmana
Mpewe mengi
malai, neema kila aina,
Muishi
hamfubai, muwapate wema wana,
Kwaheri
ya kuagana, Mkagile wa Mandai.
Muwasilishaji – Abdallah
Ahmad Seif - 0754 - 870196 au 0716 - 903355
Katibu Mwenezi Msaidizi UKUTA – Dodoma
Don Bosco – Ngozi –
Burundi
31/8/2012
Umuhimu wa Kiswahili katika jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMA)
Mada hii iliwasilishwa katika kongamano la Kiswahili lililoandaliwa
na CHAWAKAMA na CHAWAKIRWA lililofanyika
mjini Kigali Novemba 12-16 2008. Imeandikwa na Cyprian Niyomugabo, PhD
katika Sayansi za Kiisimu (Lugha za Kafrika). Mhadhiri wa Kiswahili katika chuo
kikuu cha Kigali-Rwanda (KIE).
UTANGULIZI
Si rahisi kuzungumzia umuhimu wote wa jambo lolote lile, na hivi
ni vigumu kutaja umuhimu wote wa Kiswahili mnamo dakika hizi 15 ninazopewa,
lakini nitajaribu. Kiswahili ni lugha ya kiafrika ambayo ni maarufu sana humu Afrika na nje ya bara la
Afrika. Asili ya lugha hii ni Afrika ya mashariki sehemu za mwambao au upwa
(pwani) wa Afrika ya Mashariki kando kando ya bahari ya India. Kiswahili ni
lugha yenyewe na watu wake ni Waswhili na utamaduni na utu ni Uswahili.
1. FASILI YA KISWAHILI
Kiisimu, lugha ni mfumo wa sauti nasibu za binadamu (sauti
hizo ni herufi: vokali/irabu na konsonanti). Kiisimu jamii, tutasema ya kwamba
lugha ni chombo cha mawasiliano katika jamii za binadamu. Kuwasiliana kwenyewe
ni kupashana habari kwa kutumia maneno yaani lugha.
ü Kiswahili ni lugha: ni mfumo wa sauti
nasibu, vilevile chombo cha mawasiliano kama lugha yoyote ile.
ü Asili ya Kiswahili ni Afrika ya
Mashariki: Ingawa kitovu cha Kiswahili ni Afrika ya Mashariki, kiwakati uliopo
Kiswahili ni cha sisi sote.
ü Kiswahili ni lugha ya Kiafrika. Namba
yake ni G40 katika tipolojia/ uainishaji wa lugha ya AE Meeussen.
ü Kiswahili ni lugha ya taifa nchini
Tanzania, nchini Kenya na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
ü Kiswahili ni lugha rasmi nchini
Tanzania, nchini Kenya, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika umoja
wa Afrika ( na bado haijawa lugha rasmi katika JAMA).
ü Kiswahili ni lugha ya umahiri maana
lugha iliyovuka mipaka ya kitaifa na kuwa lugha ya kimataifa. Kama asemavyo
Calvet (1988:14), “lugha inayozidi kuongeza idadi ya wazungumzaji wake na idadi
ya dhima zake ni jumuia lugha inayotapakaa”. Leo Kiswahili kinasemekana kuwa ni
lugha ya saba katika lugha za ulimwengu na ni lugha inayoongewa na takribani
watu zaidi ya milioni 100.
2. DOKEZO LA KIHISTORIA: MUHTASARI WA HISTORIA YA KISWAHILI KATIKA JAMA
Nianzie labda kwa porojo isemayo ya kwamba Kiswahili kilizaliwa
Unguja (Zanzibar), kikakulia na kulelewa Tanganyika (Tanzania Bara), kikapatwa
na ugojwa huko Kenya, kikalazwa hospitali na kufia Uganda na kuzikwa Zaire
(Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya sasa hivi) na tuongeze labda kikafufukia
hapa Rwanda leo hii. Ni porojo ambayo inaukweli wake kihistoria.
Wakati wa harakati za uhuru wanasiasa walijaribu sana kutumia
Kiswahili kama kiungo kati yao na wananchi.
TANZANIA: TAA (Tanganyika African Association) chama hiki
kilianzishwa DSM na kusambaa nchi nzima. Chama hiki kilikuwa na katiba yake
katika Kiswahili. Kiswahili kikatiliwa mkazo sana. Mnamo mwaka 1954 TAA
kikabadiliswa na kuwa TANU (Tanganyika African National Union) na kiongozi
akawa Mwalimu J.K Nyerere. Mara nyingi mikutano yake ya hadhara alitumia
Kiswahili bila ya mkalimani katika juhudi zake za ukombozi. Mnamo mwaka wa 1955
kiswahili kilianza kutumiwa Bungeni na 1961 TANU kikafanya Kiswahili kuwa lugha
ya Taifa. TANU kilijaribu sana kukikuza na kukitumia Kiswahili na watu wakaanza
kujivunia lugha hii. Wakati wote huu Kiswahili kilikuwa ni chombo muhimu cha
ukombozi wa kisiasa nchini KENYA:
Nchini Kenya Kiswahili kilipigwa vita sana na magavana wa
kizungu, mathalani 1900 Sir Charles Elist aliyekuwa Gavana alihimiza lugha za
makabila mengine na hakutaka Kiswahili kitumiwe. Lengo lake kubwa ni kuifanya
Kenya iwe chini ya wazungu na kusiwe na kiungo chochote cha lugha ya kiafrika.
Na hali hii ya kukipiga vita iliendelea sana na mnamo mwaka wa 1935 Kiingereza
kikawa ndiyo lugha ya mitihani katika shule ya msingi. Hata hivyo wanasiasa
walijaribu sana kukitilia mkazo Kiswahili toka awali na polepole kikaanza
kuwaunganisha wananchi katika harakati za ukombozi. Kumbukeni kazi ya Mhe. Rais
Jomo Kenyatta, kumbukeni kazi ya MAUMAU n.k.
UGANDA: Kiswahili ni lugha ya kwanza ya kigeni kutumiwa
nchini Uganda. Kiswahili kilianza kupendelewa na wakoloni hapo awali japo Ukristo ulikipinga maana ulikinasibisha
na Uislamu. Mathalan Gavana wa Uganda, W.F Gowers, 1927 alihimiza Kiswahili
kitumiwe Kiswahili kitumiwe Uganda huku akipingana sana na mfalme Kabaka Daudi
wa Uganda ambaye alitaka Kiganda kitumiwe, Kiswahili hata hivyo kilifahamika
bila kupata nguvu sana. Na hata katika harakati za ukombozi Kiswahili
hakikutumika sana ukilinganisha na nchi nyenzake za Afrika Mashariki.
RWANDA-BURUNDI nchini Rwanda, Kiswahili ndiyo lugha rasmi ya
kwanza ya kigeni. Mtawala Mjerumani, mfanyabiashara wa kiarabu, dini ya Islamu
na Wamisionari wa kizungu, kati ya hawa wanne si rahisi kusema ni nani ameleta
au ametumia kwanza Kiswahili nchini. Kazi nyingi zilizogusia mada hii hazikutoa
mwanga wa kutosha juu ya swali hili. Ukweli wa mambo ni kwamba Kiswahili
kiliingia rasmi Rwanda mwishoni mwa karne ya 19 wakati wa utawala wa Mjerumani.
(Taz. NIYOMUGABO C. 1992). Burundi Kiswahili kiko kwani historia ya Rwanda na
burundi wakati wa ukoloni si tofauti.
ZAIRE (DRC), Kiswahili kilisambazwa mashariki mwa Zaire na
Tiputipu (Mtipura) kabla ya 1860 akifanya safari za biashara na Kiswahili chake
kule kinajulikana kwa jina la Kingwana na ni lugha ya Taifa tena ni lugha rasmi
nchini humo.
3. UMUHIMU WA KISWAHILI KATIKA JAMA
Katika Isimujamii, lugha haichukuliwi kama mfumo
unaotenganishwa na mazingira yake ya matumizi; ndiyomaana hapa tutaona jinsi
lugha inavyofanyakazi katika jamii ya wazungumzaji wake. Kuhusu rai hii
tunasema ya kwamba luha haiwezi kuchunguzwa nje ya wale wanaoitumia kwa sababu
ni sehemu muhimu ya maisha ya watu. Mabadililko katika lugha ni sehemu moja ya
mabadiliko katika jamii nzima yaani katika utamaduni wake. Dhima ya madhumuni
ya lugha katika jamii yatakuwa mengi.
Yanayojitokeza kuwa muhimu sana ni haya yafuatayo: kusudi la kwanza la lugha
katika jamii ni kuwa chombo cha mawasiliano. Kuwasiliana kwenyewe kunatarajia
kuleta uelewano na ujirani mwema kati ya watu wa jamii au` kati ya jamii na
nyingine. Waishio katika hali ya usalama katika jamii, maendeleo yanawafikia haraka
haraka.
·
Kiswahili
ni chombo cha kujenga uhusiano, ujirani mwema
na urafiki kati ya watu na watu. Kujua lugha nyingi ni kujiongezea
uwanja wa kujipatia marafiki na kuweza kujifunza mengi kutoka kwao. Ni chombo
cha kuleta amani na utulivu kwani na amani ni mojawapo ya msingi wa maendeleo
katika jamii yoyote ile. Na kama tunaoimba katika Kanisa ni kwamba kunako
urafiki, upendo na uhusiano Mungu yupo. Sasa Mungu yu hapa katika kongamano hili.
·
Kiswahili
ni chombo cha elimu: kwa kupitia mfumo wa elimu za kijadi au za kisasa.
·
Kiswahili
ni chombo cha starehe na burudani: nyimbo zinazopendwa katika Kiswahili, kuweza
kufanya utalii kwa kutumia Kiswahili.
·
Kiswahili
ni silaha ya ukombozi na kitambulisho cha Waafrika: Tazama kazi iliyofanywa na
TANU, MAUMAU, maandishi ya Shaaban Robert katika pambo la lugha, “Titi la mama
”. titi hilo ni lipi? Ni Kiswahili.
·
Kiswahili
ni kiungo cha Waafrika: Kwa Waafrika kusini mwa jangwa la Sahara, matumizi ya
lugha za kigeni yamekuwa yakikuzwa kwa sababu mbalimbali mojawapo ni kukosekana
lugha ya kuunganisha watu wengi wa makabila tofauti.
·
Kiswahili
lugha isiyo na ukabila: Ukabila, maana , matendo au mawazo ya mtu yaliyotawaliwa
na kuthamini kabila lake tu na kubagua makabila mengine, ni kizuizi kikubwa
sana kwa maendeleo ya Afrika. Kwa hiyo Kiswahili kimekuja kama lugha ambayo
haina mwenyewe kiukabila kwani ni ya sisi sote.
·
Kiswahili
hupatia watu kazi: wakalimani wa Kiswahili katika UA, walimu, wauza vitabu,
wanahabari.
·
Kiswahili
chombo cha maendeleo: Sheila Ryanga Kenyatta University amesema: “Kila lugha
yoyote ile katika kila taifa iwe ni ya umahiri, iwe inatumika kwa uchache
inadhima yake na nafasi yake kama chombo cha maendeleo ya nchi upande wa uchumi
uongozi bora…..”. Hadhi na thamani ya lugha hutokana na hadhi ya wazungumzaji
wake. Lugha ya watu maskini hadhi yake itakuwa ya umaskini. Lugha ya watu tajiri kimaendeleo,
kiutamaduni, kiteknolojia,….itakuwa ni lugha yenye hadhi kubwa. Kwa hiyo ili
tuendeleze Kiswahili ipasavyo lazima sisi wanachi wa JAMA tufanye kazi, tutumie
bidii sana kwa kusoma hasahasa nyie vijana kwani ukesho wa JAMA ni nyie. Kama
asemavyo Mnyarwanda utakachokula kesho unakitayarisha leo.
4. MIKAKATI YA KUKUZA KISWAHILI KATIKA JAMA
Taasisi za dola zinazohusika na
ukuzaji wa Kiswahili katika JAMA inapaswa kukutanika pamoja kwa shuguli ya
kueneza lugha ya Kiswahili na huu ni wakati mzuri wa kuchunguza sera za JAMA
kiwakati uliopo katika harakati za utapakazaji wa Kiswahili. Hatua ya kwanza ya
kuweza kufikiri juu ya ukuzaji wa lugha fulani ni kujua waziwazi umuhimu wake.
Umuhimu wa Kiswahili katika JAMA unajulikana kinagaubaga. Yafuatayo ni kama
mapendekezo:
·
Kiswahili
kiwe chombo cha kisiasa cha kweli: Utambulisho wa Waafrika: Mhe. Rais Joaquim
Chissano wa Msumbiji (Rais mstaafu) ndiye Rais wa kwanza kuhutubia kikao cha
wakuu wanchi wanamemba wa Umoja wa Afrika (AU) katika Kiswahili. Wakati huo
alikuwa mwenyekiti wa umoja huo. Niwakumbushe ya kwamba kabla ya hotuba yake
katika Kiswahili, lugha rasmi za UA zilikuwa Kiarabu, Kifaransa, Kingereza na
Kireno. Alipozungumza katika Kiswahili na alikuwa anafanya ukalimania yeye
mwenyewe. Wakati Rais Chissano alipozungumza Kiswahili kwa mara ya kwanza
viongozi wengi na hata mabalozi walipatwa na mshangao na tangu wakati huo
azimio likachukuliwa ili Kiswahili kiwe mojawapo ya lugha rasmi za umoja huo.
Na sasa hivi Rais Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amabaye amechukua uenyekiti wa UA
kutoka kwa mwenyekiti aliyemaliza muda wake Rais John Kufor wa Ghana
aliwahutubia wakuu wenzake katika Kiswahili mnamo kikao cha mwisho cha mwezi
Januari 2008. Hatua za Marais hawa zilikanganya wenzao kwani ilkuwa mazoea kwa
wakubwa wa Afrika kutumia lugha za kigeni na kuonyesha umahiri na ubingwa wao
katika lugha hizo za kigeni. Nikumbushe kwa kupitia ya kwamba mpaka sasa hivi
kwa mujibu wa katiba ya JAMA lugha ya Kiingereza ndiyo lugha rasmi inayotumiwa
na Kiswahili kimeelekezwa kutumika kama lugha ya mawasiliano, ambapo jitihada
za kukifanya kiwe lugha rasmi zinaendelea. Hapa kuna maoni tofauti: (a)
Kiswahili kiwe lugha ya JAMA peke yake tu. (b) Kiingereza kiwe peke yake lugha
rasmi katika JAMA. (c) Kiswahili na Kiingereza, lugha hizi mbili zichukuliwe
kama lugha rasmi za JAMA. Hali ya uwili lugha (hali ya ulugha mbili) au ulumbi
(ulugha nyingi) iingizwe katika JAMA (mfano
Kiswahili-Kiingereza-Kifaransa/Kiswahili-Kiingereza/Kiarabu….). Nyie mnaonaje?
Mnipashe. Mimi maoni yangu ni yafuatayo:
·
Sera
ya lugha na upangaji wa lugha: Sera ya lugha ni taratibu mbalimbali za kuratibu
matumizi ya lugha katika jamii. Upangaji wa lugha ni jitihada za kuweka sera
mbalimbali za lugha ambao husaidia kutatua tatizo la mawasiliano katika jamii.
Tunajua ya kwamba mradi wa upangaji wa lugha si jambo rahisi. Kwani kweli sera
ya upangaji wa lugha katika jamii/jumuia fulani huonekana mara nyingi kama
jaribio gumu kwani inazingatia uteuzi wa kiitikadi na kutilia maanani maoni ya
kijamii, kistadi na kiutekelezaji. Wakati umefika ili kuwepo sera ya nafasi ya
kila lugha katika JAMA maana kuonyesha nafasi ya kila lugha kufuatana na
umuhimu au dhima zake katika jamii. Kudhihirisha nafasi za lugha za kiasili
(makabila/makundi), lugha za taifa, lugha za ukanda, lugha za kimataifa. Ingawa
Kiswahili kimefikia hatua ya lugha inayozungumzwa na wengi na yenye dima nyingi
katika JAMA, si kumanisha kuwa hakuna vipingamizi vya uenezaji wake. Kizuizi
chake cha kwanza ni mapambano ya kilugha. Taasisi za dola zinazojihusisha na
ukuzaji wa lugha ya kiswahili zifanye kazi bega kwa began a ACALAN (African
Academy of Languages) maana Akademia ya lugha za Afrika ya UA.
·
Kiswahili
kiwe chombo cha elimu cha kweli: Kiswahili kiwe chombo cha kufundishia katika
viwango vyote vya masomo lakini tusisahau na lugha nyingine. Taz. Upangaji
lugha.
·
Kufuta
kasumba za ukoloni: kasumba ni mabaki ya fikra za kikoloni kichwani mwa mtu.
Kuna waafrika wengi sana ambao wanafikiri ya kwamba kujua au kuzungumza lugha
za kiafrika, lugha za kishenzi, lugha duni, lugha za akinayake, lugha ambazo
ndani yake kuna umasikini… ni aibu na ni kukosa akili. Mhe George Mkuchika
(Mb), Waziri wa Habari utamaduni na michezo, Tanzania, akizungumzia kuhusu
ukuzaji wa lugha ya Kiswahili na lugha za kiafrika kwa ujumla amesema “Mada hii
ni mada muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho nchi zetu za kiafrika
zimekwishajipatia uhuru wa kujitawala na kujiamulia mambo yetu wenyewe na
kwamba kazi kubwa iliyoko mbele yetu kwa sasa ni kuelekeza jitihada zetu katika kujikomboa
kifikira, kiutamaduni na kiuchumi mambo ambayo yalikandamizwa na kudidimizwa
wakati wa kipindi cha ukoloni, kwa hiyo kwa kupitia dini na utawala
walijitahidi kuwatia wenyeji kasumba ili waone kila walichonacho ni cha
kishenzi; kuanzia lugha, dini, utamaduni, teknolojia, dawa na mengineyo. Somo
hili walilotoa lilifanikiwa sana na likawa ni sehemu au viambajengo vya ukoloni”.
Kwa wakati mwingi mradi wa kukuza lugha za kiafrika kwa jumla na kiswahili
hasahasa hupingwa kwa sababu idadi ya watu wengi wanaochukua madaraka katika nyanja
mbalimbali za taifa walisomea katika mfumo wa ufundishaji wa kikoloni. Baadhi
ya hawa ni watu ambao machoni mwao kuwa na mradi wa kukuza lugha ya kiafrika ni
upotezaji wa wakati na pesa.
·
Kutafsiri
vitabu na maandishi mengine katika Kiswahili: Ili Waafrika wa kila kiwango cha
ujuzi wanufaike na maendeleo ni lazima ujuzi wote (teknolojia, sayansi,
falsafa…) viwekwe katika Kiswahili kutoka lugha ambazo jamii zake zimepiga
hatua kimaendeleo kama Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kidachi, Kijapani n.k.
Vilevile ni lazima kazi za uandishi na utangazaji wa vitabu na utafiti wa kila
aina katika Kiswahili yatiliwe maanani. Kwani kama asemavyo Senkoro (1987) “elimu
na maarifa mbalimbali ni mali ya watu wote duniani”.
·
Kuweka
nguvu zaidi katika utungaji kamusi na ukuzaji wa istilahi. Ili lugha iwe na
uhai lazima iweze kutafsiri dhana zote na fikra zote katika lugha hiyo ili
iweze kuwa chombo cha kweli cha maendeleo ya kila aina. Kwa upandea wa
Kiswahili tunapongeza sana kazi iliyofanywa na TUKI pamoja na BAKITA.
·
Kufungulia
milango “viswahili” vingine. Kiswahili sanifu lazima kifungulie milango launi
nyingine ya Kiswahili hasahasa cha Afrika ya Kati.
·
Kuongezeka
idadi ya makongamano kuhusu ukuzaji wa Kiswahili kwa ngazi ya kitaifa na
kimataifa.
ASANTENI
NYOTE!
MAREJEO
Calvet, L.J. Les langues vehiculaires, PUF, Paris, 1981.
Chimerah, R.M. Kiswahili past present and future Horizons,
Nairobi 2009.
Kagabo, J.H.L. Islam et les “Swahili” au Rwanda, Paris, 1988.
Khalid Abdallah, the liberation of Swahili, Nairobi, 1977.
Massamba, D.P.B. Historia ya Kiswahili 50BK hadi 1500 BK,
Nairobi, 2002.
Mmallavi, A.P.W. Lugha katika jamii, EAPH, DSM, 1977.
Niyibizi, S. Le Swahili au Rwanda: Aspects historique,
linguistique et sociolinguistique, Butare 1980.
Niyomugabo, C. Nafasi ya lugha ya Kiswahili katika uwanja wa
dini nchini Rwanda: Mkabala wa kiisimujamii, Ruhengeri 1992.
Senkoro, F.E.M.K. Fasihi na jamii, DSM, 1987.
Shihabudin Chiragdin na M. Mnyampala (1977) Historia ya
Kiswahili OUP, Nairobi.
Tuli R.S.K. (1985) Chimbuko la Kiswahili kukua na kuenea
kwake, Arusha Tanzania.s
Asante wana UKUTA kwa uchaguzi mlioufanya kwani hii ndio demokrasia inayotakiwa, pia nawakumbusha viongozi kuwa umoja ni nguvu na kama atakuwepo kiongozi msaliti basi ajing'oe kabla hatamg'oa napenda mashairi wala si utani kwangu Kiswahili ni Tunu. nitakirumba popote pale wakti wa shida na wakati wa raha pia.
ReplyDeleteSafari huanza kwa hatua ya kwanza. Kiswahili kitaweza siku moja kuwa lugha rasmi katika eneo la Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, siku moja!
ReplyDeleteTukiendeleza juhudi za kukitangaza na kukikuza kitafikia lengo la kikanda hata afrika kwa ujumla
ReplyDelete