Shukrani
Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa wale wote
walioshirikiana nasi hadi kufanikisha kuhudhuria kongamano hili. Kwa kweli
ilikuwa ni changamoto kubwa kufanikisha kuhudhuria katika kongamano kutokana na
uhaba wa pesa tulio nao. Pamoja na changamoto hizo lakini uongizi wa chawakama
ulithubutu kumpeleka kiongozi mmoja ili kuwakilisha tawi letu, tunawashukuru
sana.
Vilevile tunawashukuru sana wanachama waliojinyima
na kuamua kutumia pesa kwenda MUCE ili kuwakilisha tawi letu, mmetujengea
heshima kubwa, tunawashukuru sana.
Mwisho kabisa tunapenda kumshukuru Katibu msaidizi
kwa moyo wake wa kujitolea, kutokana na ukata unaoukabili CHAMA, aliamua
kutumia pesa zake ili kufanikisha kuhudhuria katika kongamano.
Utangulizi
CHAWAKAMA-UDSM imekuwa mstari wa mbele katika
kuhakisha malengo ya chama yanasonga mbele. Uwakilishi wetu katika makongamano
umekuwa ni mzuri sana. Tangu kongamano la kwanza (1) la kanda hadi hili la sita
(6) tumekuwa na uwakilishi katika kila kongamano, japokuwa idadi ya wawakilishi
inakuwa ndogo lakini angalau tunakuwa na uwakilishi.
Kwa kuzingatia mlolongo huu wa kuandaa makongamano,
kongamano la 6 limefanyika katika Chuo Kikuu kishiriki Cha Mkwawa (MUCE). Kama
ilivyokawaida yetu sisi CHAWAKAMA-UDSM katika kutimiza majukumu muhimu ya
chama, tulituma uwakilishi katika kongamano hili. Jumla ya washiriki kutoka
tawi letu waliohudhuria ni wanne (4). Kiongozi mmoja na wanachama wa kawaida
watatu. Idadi hii ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanachama zaidi ya
100 tulionao lakini sababu pekee ya idadi hii ni kutokana na uhaba wa pesa
tulionao.
Kwa hiyo ripoti hii ina lenga kuelezea kile
kilichojiri katika kongamano la 6 lililofanyika MUCE-Iringa.
KONGAMANO LENYEWE
Kongamano la 6 la kitaifa la CHAWAKAMA mwaka 2013
lilifanyika katika chuo kikuu kishiriki cha Mkwawa (MUCE) – Iringa. MUCE ndio
walio kuwa wenyeji wa kongamano la 6 mwaka 2013.
Washiriki kutoka vyuo mbalimbali vya Tanzania
walihudhuria ikiwa ni pamoja na washiriki kutoka shule ya Sekondari Mlamke.
Washiriki wa kongamano walianza kuwasili tarehe 20 Feburuari kutoka katika vyuo
mbalimbali kutoka maeneo tofautitofauti ya Tanzania. Miongoni mwa vyuo hivyo
Chuo kikuu cha Dar es Salaam hakikuwa nyuma na kiliwakilishwa na wanachama wanne.
Baada ya kuwasili tulikaribishwa kwa bashasha na wenyeji wetu na siku hiyo
ilikuwa ni siku ya maadalizi kwa ajili ya ufunguzi rasmi wa kongamano.
Tarehe 21 Feburuari ndio ilikuwa siku rasmi ya
ufunguzi wa kongamano. Kabla ya kuingia ukumbini asubuhi ya siku hiyo kwa ajili
ya ufunguzi rasmi tulifanya maandamano kwa kuimba nyimbo za kukitukuza Chama
chetu. Baada ya kuingia ukumbini tuliketi chini na kumsikiliza Manju ili kujua
kile kilichokuwa kinafuata kwa mujibu wa ratiba ya siku hiyo.
Ilipotimia saa 3 asubuhi kongamano lilifunguliwa
rasmi. Mgeni rasmi wa kongamano alikuwa ni Makamu Meya (Deputy Mayor) wa
Manispaa ya Iringa Ndugu Gervance Ndaki ambaye alikuja kwa niaba ya Mkuu wa
mkoa wa Iringa.
Baada ya ufunguzi huo ilifuata risala iliyosomwa na
Mwenyekita wa Kanda ya Tanzania kwa mgeni rasmi. Risala hiyo ilihusu maendeleo
ya chama kwa ujumla ambayo ni mazuri ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo
Kiswahili hakikuwa na hadhi ya juu ukilinganisha na sasa ambapo tunaona
Kiswahili kimenea na kukua kwa kasi sana. Pamoja na mafanikio hayo pia risala
ilionesha jinsi chama kinavyokabiliwa na changamoto. Changamoto hizo ni pamoja
na uhaba wa fedha kwa ajili ya kuendeshea chama, kwa mfano kushindwa kuandaa
makongamano kwa fedha za chama na badala yake tunategemea malipo yanayofanywa
na wanachama, hii inamaana kwamba bila wanachama kuchangia hatuwezi kuandaa
kongamano. Pia kutokana na uhaba wa fedha chama kimeshindwa kusajiliwa mpaka
hivi sasa kitu ambacho ni tatizo kubwa kwa kutotambulika kwa chama chetu
kisheria.
Hongereni CHAWAKAMA DAR. kwa kuwa na chanzo hiki muhimu cha kuwasiliana nawatakia kazi njema viongozi wote katika kulisukuma gurudumu hili kwa umoja wala msiuruhusu utengano ukapenya miongoni mwenu. Kweli Kiswahili ni Tunu na Johari ya Afrika.
ReplyDelete