MNAMO TAREHE 26/02/2014
HADI TAREHE 1/3/2014.
1.0
Utangulizi.
Chama
cha Wanafunzi wa Kiswahili Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) kilianzishwa mwaka 2004
ambapo pamoja na malengo mengine, lengo kuu ni kukuza na kueneza lugha ya
Kiswahili Afrika na Duniani kwa ujumla. Ikiwa kama sehemu ya lengo la chama;
makongamano mbalimbali huandaliwa kwa utaratibu maalumu ndani na nje ya nchi
kwa lengo la kuwaweka pamoja wanachama na wadau wengine wa lugha ya Kiswahili
ili kuwatia chachu ya kuendeleza lugha hii adhimu na haushi.
Utaratibu
wa uandaaji wa makongamano upo katika mawanda ya kimataifa (jumuiya) na kitaifa
(kikanda) ambapo katika mawanda ya kijumuiya huhusisha nchi za jumuiya ya
Afrika Mashariki hivyo kwa kufuata muundo wa uandaaji, Kongamano la mwaka huu
limepangwa kufanyika nchini Kenya. Kwa upande wa ndani ya nchi, makongamano
haya hufanyika ndani ya nchi husika ambapo kongamano la mwaka huu liliandaliwa
na kufanyika katika chuo kikuu cha Eckenforde mjini Tanga
1.1 Kongamano lenyewe.
1.1.1 Washiriki
Katika
kongamano hili jumla ya washiriki wanachama 280 walihudhuria wakiwemo wahadhiri
na wadau wengine wa lugha ya Kiswahili kutoka katika Vyombo vya habari, waalimu
wa shule za sekondari na viongozi wa kiserikali. Pia baadhi ya mabwiji wa lugha
hii walishiriki wakiwemo Prof. Msanjila, Mwansoko(aliyekua mgeni rasmi),
Kiango, na Prof Senkoro
1.1.2
Uwasilishaji Mada
Mada
zote zilizopendekezwa ziliwasilishwa. Mada hizo ni Mchango na changamoto za
vyombo vya habari, Bunge na Wanataaluma katika kukuza na kueneza lugha ya
Kiswahili hapa nchini. Nini suluhisho la changamoto hizo?, lugha ya Kiswahili
ni bidhaa adimu, jadili ni jinsi gani kijana atakavyoitumia kuleta maendeleo
endelevu., Sharban Robert kama baba wa fasihi ya Kiswahili anayo nafasi gani
katika fasihi ya zama hizi? na mchangamano baina ya asili ya Kiswahili na
Mswahili.
1.1.3
Kauli Mbiu
Kauli
mbiu ya mwaka huu ilikua ni MIAKA 52 YAUHURU, KISWAHILI TUNU YA KIJANA KWA
MAENDELEO ENDELEVU. Kauli mbiu hii inamtia kijana hamasa ya kutumia lugha ya
Kiswahili vyema katika kujiletea maendeleo yanayodumu.
1.1.4
Siku ya kwanza.
Siku
hii ilianza kwa namna yake ambapo washiriki wote wakiongozwa na kikundi cha
tarumbeta waliingia ukumbini kwa maandamano ya matembezi mafupi kiasi cha robo
kilometa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi. Baada ya kuwasili ukumbini
washiriki pamoja na wageni walichukua nafasi zao ambapo utambulisho ulifanyika
kasha risala ikasomwa na mwenyekiti wa CHAWAKAMA kanda Erasto Chan’ga na
kufuatiwa na hotuba kutoka kwa mgeni rasmi Profesa Mwansoko. Baadaye
tulipata ‘CHAASU’ kisha ikasomwa mada ya kwanza kutoka chuo wenyeji na kuchangiwa na washiriki mbalimbali. Baada ya
hapo tulipata CHAMCHA kisha mada moja binafsi ikasomwa na kuchangiwa na baadhi
ya wadau waliokuwepo. Baada ya wasilisho
la mada hiyo ilifuatiwa na vitushi mbalimbali kutoka kwa wanachama hatimaye
muda wa chajio nakufuatiwa na wasaa binafsi.
1.1.5
Siku ya pili.
Tulikutana
ukumbini saa mbili kama ilivyo ada, kisha mada ya Mchangamano baina ya asili ya
Kiswahili na Mswahili iliwasilishwa na wanachama kutoka chuo kikuu cha Zanziba
SUZA na kuchangiwa na wadau mbalimbali. Baada ya hapo ilifuatia mada ya Shaban
Robert kama baba wa fasihi ya Kiswahili na nafasi yake katika zama za hivi leo.
Wasilisho liliandaliwa na kuwasilishwa na wanachama kutoka chuo kikuu cha Dar
es Salaam ambayo iiwasilishwa makusudi kwa lengo la kujua wasifa wa nguli huyu
kabla ya kwenda kuzuru makazi yake. Baada ya kupata ‘chai nzito’ tulienda kuzuru nyumbani kwake
(Machui) alipoishi na kuzikwa nguli wa fasihi Shabani Robert. Baada ya kufika
kwenye makazi yake tuliwakuta wenyeji akiwemo mama mdogo wa marehemu pamoja na mjukuu wake aliyetusimulia habari
zake. Pamoja na kuzuru alipozaliwa, pia tulizuru mahali alipoishi, maktaba na
alipopumzikia na kuuza machapisho yake maeneo ya ufukwe wa bahari ya hindi.
Waaida Chama kwa kupitia harambee ndogo iliyofanyika, kilitoa zawadi ya vyakula
vyenye thamani ya shilingi laki moja na sitini elfu (160000) kwa ndugu zake
marehemu. Baada ya kurudi ukumbini tulipata burudani kisha Chajio na hatimaye
uhuru binafsi.
1.1.6
Siku ya tatu.
Mada
ya nne iliyokua inahusu mchango na changamoto za vyombo vya habari, Bunge, na
Wanataaluma katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili hapa nchini
iliwasilishwa kisha kuchangiwa na washiriki mbalimbali akiwemo mwandaaji wa
vipindi vya Kiswahili TBC1 Victor Eliah ambaye pamoja na michango mingine
alitoa wito kwa wanachawakama kushiriki katika kutangaza lugha ya Kiswahili
kupitia runinga kwani nafasi zipo. Ilifuata chai nzito kabla ya safari ya
kuzuru kwenye mapango ya kihistoria ya Amboni ambapo tuliona na kujifunza mengi
kuhusu utamaduni wetu. Tuliporudi ukumbini tulipata wasaa wajiliwaza kwa
burudani ambapo fursa ya kucheza na kughani mashairi ilitolewa, muda wa Chajio
ulipowadia washiriki walijipatia na wasaa wakujinafasi ulifuata.
1.1.7
Siku ya nne.
Kama
ilivyodesturi kwa wakazi wa mji wa Tanga wa kufanya kazi ya usafi kwa pamoja
kwa kila jumamosi ya kila mwisho wa mwezi, nasi hatukubaki nyuma kwani kitu
kizuri kula na mwenzako, wanatanga walitualika ambapo pamoja na wakazi wengine
mkuu wa wilaya ya Tanga Mjini alitupa shavu. tulishiriki usafi katika eneo la
kiwanja cha mpira wa miguu cha Mkwakwani pamoja na maeneo yaliokizunguka.
Baada
ya usafi, wanachama walienda ufukweni kuzuru eneo ambalo Shaban Robert alikua
anauzia machapisho yake, wakapata ‘chai nzito’ huko ambapo viongozi wote wa
matawi, kanda na wa Afrika Mashariki walikua na kikao eneo jirani na hilo. Kama
wanenavyo wahenga hakuna marefu yasiyokua na ncha, ilpotumi saa sita mchana
tulirudi ukumbini na ilipojiri saa saba mchana Profesa Mwansoko alitamatisha kongamano la
tisa la CHAWAKAMA kitaifa kwa nasaa yake
fupi iliyotamalaki hekima za kitaaluma.
2.1
Mafanikio.
Kutokana
na yaliyojiri katika kongamano, kama ilivyoripotiwa hapo juu ni wazi kwamba
limeacha alama za ushindi na funzo kwa wangenzi walioshiriki.
2.1.1
kongamano hili limetoa nafasi ya kipekee kwa wadau washiriki kumjadili kwa kina
aliyekuwa mwandishi wa kazi za kifasihi hayati Shaban Robert kwa njia ya makala
na uwandani.
2.1.2
Kongamano hili limefanikiwa kuwa kongamano la kihistoria kwani wanachama
waamefanikiwa kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria kama vile kwenye
Mapango ya Amboni.
2.1.3
Pia kongamano limeamsha ari kwa wadau mbalimbali wa Kiswahili katika kuendeleza
na kukuza lugha ya Kiswahili popote Duniani kwani lilifanikiwa kuwaweka pamoja
wadau wote wa lugha ya Kiswahili na kuwatia hamasa ya kueneza lugha hii ya
Kiswahili.
2.1.4
Uwasilishwaji wa mada umejenga changamoto kwa wanagenzi wa lugha hii adimu
kubuni na kurekebisha makosa katika kukiendeleza Kiswahili. Kwa mfano mada ya
changamoto za wa Bunge, Wanataaluma na Vyombo vya habari linatoa nafasi kwetu
kama wanataaluma kuboresha lugha yetu katika Nyanja tajwa.
3.1
Changamoto.
Kama
wanenavyo wahenga ‘Hakuna kapa isiyokuwa na usubi’ Pamoja na kuwepo kwa
mafanikio makubwa katika kongamano hilo, pia kulikua na baadhi ya changamoto.
3.1.1
Changamoto hizo ni pamoja na kutokuwepo kwa sehemu nzuri za malazi. Mazingira
ya kulala yalikua ni shida kwani baadhi ya
watu hawakuzoea kulala kwenye mazingira kama yale na hivyo kusababisha kwenda
kulala kwenye vyumba vya wageni kwa gharama zao.
3.1.2
kutokujitosheleza kwa ratiba ambapo baadhi ya matukio yaliyooneshwa kufanyika,
hayakufanyika. Kwa mfano, ratiba ilikua inaonesha kungekuwepo na burudani
kutoka kwa wasanii kama akina Mrisho Mpoto pamoja na Mzee Majuto lakini
hatukufanikiwa kuwaona wala kupata burudani kutoka kwao.
4.1 Mapendekezo.
Mambo
yafuatayo yanapendekezwa ili kuboresha makongamano yajayo;
4.1.1
Suala la malazi liandaliwe
na kudhibitisha ubora kabla ya siku ya kongamano.
4.1.2
Matukio yatakayokua
yameandikwa kwenye ratiba yawe yamethibitishwa kwamba yatakuwepo.
IMEANDALIWA NA ABEL
PATRICK- KATIBU CHAWAKAMA CKDSM
IMEHARIRIWA NA ATHANAS BARNABA- MHARIR
CHAWAKAMA CKDSM
Napenda kuwapongeza CHAWAKAMA CKDSM kwa juhudi zenu mnazozifanya za kueneza lugha ya Kiswahili kwa njia ya makongamano, nimatumaini yangu kuwa mtakuwa wenyeji wa kongamano lijalo. Ahsanteni.
ReplyDelete